Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Timu ya Simba imepangwa kucheza na Red Arrows ya Zambia katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika kuwania kutinga makundi ya michuano hiyo baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wekundu wa Msimbazi hao wanatarajia kuanzia nyumbani, Novemba 28, marudio Desemba 5, mwaka huu.
Simba ilitolewa na Jwaneng Galaxy ya Botswana baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-1 nyumbani huku ikiwa imetoka kushinda 2-0 katika mchezo wa kwanza ugenini.
Kipigo hicho ambacho hakikutarajiwa na mashabiki wa kikosi hicho, kilivuruga hali ya hewa hadi Kocha Mkuu wa Didier Gomes kufikia hatua ya kuchana na klabu hiyo.
Tofauti na Gomes, klabu ya Simba imesitisha mikataba wa kocha viungo Adel Zrane na mwalimu wa makipa Milton Nienov.
Aidha uongozi wa Wanamsimbazi hao, umemkabidhi jukumu ya kuwa kocha mkuu wa muda Thierry Hitimana ambaye atasaidiwa na Selemani Matola.