28.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA, YANGA VITANI Z’BAR LEO

yanga-na-simba

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

MACHO na masikio ya mashabiki wa mchezo wa soka, leo yatakuwa katika Uwanja wa Amaan mjini Unguja, kufuatilia pambano la nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi baina ya timu kongwe za Simba na Yanga.

Timu hizo zinakutana katika nusu fainali ya pili itakayochezwa majira ya saa 2:15 usiku, baada ya mchezo wa nusu fainali ya kwanza ambayo itazikutanisha Azam FC dhidi ya Taifa  Jang’ombe kupigwa kuanzia majira ya saa 10:15 jioni.

Simba wanaoongoza katika Kundi B kwa kufikisha pointi 10, watakutana na watani wao wa jadi Yanga wanaoshika nafasi ya pili Kundi A, huku Azam ambao ni vinara wa Kundi A wakivaana na Taifa Jang’ombe waliopo nafasi ya pili Kundi B.

Timu hizo zinakutana katika hatua hiyo baada ya Simba kuinyuka Jang’ombe Boys mabao 2-0, wakati Yanga ilijihakikishia kucheza nusu fainali mapema licha ya kuchapwa mabao 4-0 na Azam.

Hii ni mara ya tano kwa timu hizo kongwe kukutana katika ardhi ya Zanzibar zikicheza  michuano tofauti, huku michuano ya Kombe la Mapinduzi ikiwa ni mara ya pili tangu walipokutana mwaka 2011.

Katika mechi nne ambazo timu hizo zimekutana, Simba wameonekana kuwa na historia nzuri ya kushinda mara tatu huku mahasimu wao Yanga wakishinda mara moja.

Hata hivyo, Yanga watavaana na Simba wakiwa wamepania kuendeleza ubabe na rekodi yao ya ushindi kama walivyofanya katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.

Msimu uliopita Yanga walishinda mabao 2-0 dhidi ya Simba katika mzunguko wa kwanza na kufanikiwa kutoa kipigo kingine kama hicho walipokutana kwenye duru ya pili, lakini msimu huu walitoka sare ya bao 1-1.

Akizungumzia mchezo wa leo, Kocha mkuu wa Simba, Mcameroon Joseph Omog, alisema anafahamu ugumu wa mechi hiyo kwani mara nyingi timu hizo zinapokutana zinakuwa zimejiandaa vizuri na kukamiana, huku akisisitiza kuwa matarajio yao ni kutinga hatua ya fainali.

“Nashukuru tumefanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali, lakini tutapambana kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi ili kupata pointi tatu muhimu licha ya mchezo huo kuwa wa ushindani mkubwa,” alisema Omog.

Naye kocha mkuu wa Yanga, Mzambia George Lwandamina, alisema kwenye soka lolote linaweza kutokea, hivyo wamejipanga kuhakikisha wanashinda mchezo wa leo na kutinga hatua ya fainali baada ya kuyafanyia kazi makosa yaliyosababisha wafungwe na Azam mabao 4-0.

Kipigo cha Yanga katika mchezo dhidi ya Azam kilisababishwa na washambuliaji wake kukosa umakini katika ufungaji pamoja na udhaifu wa safu ya ulinzi ambayo haikuwa imara.

Kwa upande wake kocha msaidizi wa Azam, Iddy Cheche, alisema malengo yao ni kutwaa Kombe la Mapinduzi mwaka huu licha ya kukabiliwa na mchezo mgumu watakapoivaa Taifa Jang’ombe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles