28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Simba na Yanga Oktoba1, Historia mpya kuandikwa

simba-na-yanga

* Mashabiki kushuhudia mbinu, ufundi na falsafa 

* Sera mpya za kuzibadili timu kuchagiza mchezo huo

NA SAMUEL SAMUEL, DAR ES SALAAM

LICHA ya kutokuwa na maendeleo makubwa ya kisoka barani Afrika, soka bado umekuwa mchezo pendwa zaidi Tanzania na kugeuka kama alama ya umoja, mshikamano na chachu ya maendeleo kijamii.

Ndani ya jamii hii umeibuka upinzani mkali, ulioibua dhana ya upinzani wa jadi katika soka.

Unapolizungumzia pambano la soka kati ya Simba na Yanga, unazungumzia pambano la watani wa jadi la tatu kwa umaarufu barani Afrika, baada ya lile la Al Ahly na Zamaleki pale Misri na Kaizer Chiefs dhidi ya Orlando Pirates kule Afrika Kusini, kwenye mji maarufu wa Soweto (Soweto Derby).

Homa ya watani wa jadi, yaani Simba na Yanga inaongezeka kila uchao kuelekea Oktoba Mosi, siku mtanange huo utakapopingwa kwenye Uwanja wa Taifa, hii ni kutokana na ubora wa vikosi vyote.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Februari 20, 2016 msimu uliopita na mabingwa watetezi, Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, mabao yaliyofungwa na Donald Ngoma dakika ya 36 kipindi cha kwanza na Amisi Tambwe dakika ya 77 kipindi cha pili.

Ukitazama uimara kimbinu na kiufundi kwa timu zote msimu uliopita kabla ya pambano lao la Februari 20, utaona Yanga walikuwa juu na Simba haikuwa vema kutoa ushindani na ndicho kilichosababisha kupoteza mechi zote mbili walizokutana.

Yanga Oktoba Mosi wanakutana na Simba mpya, ambayo ipo vizuri kimbinu na kiufundi kutokana na marekebisho makubwa waliyoyafanya kwenye kikosi chao msimu huu.

Simba wamebadili benchi lao la ufundi kwa kumleta Joseph Omog, ambaye analijua vema soka la Tanzania akiwa na rekodi ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2013/14 akiwa na Azam FC.

Hivyo si mgeni sana katika joto la watani wa jadi, anajua raha na karaha za mmoja wao kupoteza pambano hilo.

Uwepo wa Mayanja kama kocha msaidizi Simba, ambaye alikuwa kwenye benchi la ufundi msimu uliopita kama Kocha Mkuu, Simba ikilambwa 2-0, utasaidia kuwa mshauri mzuri kimbinu, kiufundi na falsafa sahihi kulipiza kisasi kwa mabingwa hao watetezi.

Muunganiko kimbinu na kiufundi kwa Simba na Yanga, katika mchezo huo utaona kabisa wapenzi wa soka msimu huu wanakwenda kushuhudia mechi nzuri na yenye upinzani halisi pande zote.

Ukiangalia usajili wa Simba, Laudit Mavugo kutoka Burundi, mwenye uwezo mkubwa wa kucheka na nyavu ni msumari wa moto kwa walinzi wa Yanga.

Blagnon toka Ivory Coast, ana fiziki ya kutosha na mzuri kucheza kama mshambuliaji namba mbili kificho, anazidi kutoa taswira ya umakini wa Simba katika usajili wa mwaka huu.

Yanga wanasifika sana kwa uimara wao wa mashambulizi ya pembeni, yanayoanzia kwa walinzi wa pembeni au mawinga wao, hususan Simon Msuva kulia na Deus Kaseke kushoto.

Msuva na Kaseke watarajie upinzani mkali kwa wekundu hao wa Msimbazi, ambao msimu huu wameongeza idadi ya viungo  wenye uwezo mzuri kukaba na kupunguza eneo la kati na pembeni kimbinu kwa kuziba sehemu zilizo wazi ‘open spaces’ ambazo huwafanya viungo wa pembeni wa Yanga au mabeki wao kupanda kwa kasi.

Shiza Kichuya na Mzamiru Yassin wanaiweza vyema kazi hiyo, hivyo walinzi wa Yanga wawe makini sana na Kichuya aliyetokea Mtibwa Sugar.

Kichuya ni kiungo makini katika ukabaji, kuchezesha wenzake lakini hatari zaidi kucheza kama kiungo mshambuliaji kificho, tayari ana goli zake mbili za maana.

Simba msimu uliopita ilikuwa inakosa wachezaji wazuri katika benchi la ufundi wenye uwezo wa kuingia ndani, ama kuendeleza kasi ya mchezo au kubadilisha mfumo wa uchezaji kimbinu kama timu imebanwa, lakini msimu huu Simba ipo vizuri na kuonekana tishio.

Kichuya, Mzamiru, Mnyate, Mavugo, Janvier Bokungu ni wachezaji wapya wanaokutana na wakali wengine, kwa uchache ni Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto, Ibrahim Ajib na nahodha Jonas Mkude. Si kwamba ubora wa Simba wamejihakikishia ushindi kwa mabingwa hao watetezi.

Yanga wenyewe katika mechi zake nne mpaka sasa imetuma salamu za tahadhari kwa wekundu hao, wana rekodi nzuri ya kutoruhusu goli lolote kugusa nyavu zake, hii ina maana wakali hao wa Jangwani wana safu nzuri ya ulinzi, tofauti na Simba walioruhusu nyavu zao kutikisika mara tatu licha kushinda.

Uimara wa Vicent Bossou na ingizo jipya Andrew Vicent ‘Dante’ katika safu ya ulinzi ni karata ya turufu kimbinu kwa Yanga mbele ya washambuliaji wasumbufu wa Simba SC.

Walinzi hao wa kati ni kombinesheni namba mbili mbele ya pacha kongwe ya ulinzi chini ya Nadir Haroub na Kelvin Yondani, hapa ndio utaona ni jinsi gani joto la watani hawa toka 1935 na 1936 linavyofukuta.

Licha ya ubora wa viungo wa Simba SC msimu huu, itawahitaji kuvuta kweli soksi zao mbele ya Deusi Kaseke, Thaban Kamusoko, Said Makapu, Haruna Niyonzima, Mahadhi Juma, Yusufu Mhilu, Pato Ngonyani na Mbuyu Twite, msitu wa viungo wazuri na wenye kasi ya ajabu.

Simba wakiwaangalia Amisi Tambwe na Ngoma ni lazima nyuzi joto za mchezo huo kwa upande wao zipande, wakikumbuka alichowafanyia msimu uliopita.

Mchezo huu kifalsafa unachagizwa na ujio wa sera mpya za kuzibadili timu hizo katika mfumo wa uendeshaji.

Tayari bilionea Mohamed Dewji amekwisha kuchukua dhamana ya kuwalipa mishahara wachezaji wa Simba kwa miezi sita, ikiwa ni sehemu ya kusakafia wazo lake la kuzitaka hisa za asilimia 51 za timu hiyo.

Ni dhahiri atawajenga vema wachezaji wa timu kisaikolojia kwa posho na ahadi nono kuelekea mchezo huo.

Manji, ambaye anakitaka kikosi cha Yanga kwa miaka 10 kwa asilimia 75, naye sidhani kama atakuwa nyuma kuisadia timu kisaikolojia kushinda mchezo huo ili thamani ya soko lake kibiashara iongezeke.

Ni mpambano mzuri endapo waamuzi watafuata sheria 17 za soka kwa usawa bila upendeleo, pia wachezaji wa timu zote kuzingatia nidhamu ya mchezo huo pendwa zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles