30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Simba yakwama kwa Mbao

   Na MASYENENE DAMIAN-MWANZA               |         

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya soka ya Simba imeshindwa kuendeleza wimbi la ushindi, baada ya kufungwa bao 1-0 na Mbao FC katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana.

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani, Simba walianza kwa kasi ambapo katika dakika ya pili, Mohamed Ibrahim, aliambaa na mpira na kuachia shuti lililowababatiza mabeki wa Mbao na kuzaa kona ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.

Simba waliongeza mashambulizi na katika dakika ya tano, Shiza Kichuya, alishindwa kutumia vema nafasi aliyoipata baada ya kupokea krosi ya Emmanuel Okwi na kuachia shuti lilipanguliwa na kipa wa Mbao, Hasheem Mussa.

Mbao walicharuka na kuanza kulishambulia lango la Simba, ambapo katika dakika ya 15, Pastory Anthanas, alishindwa kuitumia vema nafasi aliyopata kuifungia timu yake, baada ya kupiga shuti lililotoka nje akipokea pasi ya Vicent Philipo.

Katika dakika ya 17, Mwamuzi Jonesia Rukya, alimlima kadi ya njano beki wa Mbao, Ally Mussa, baada ya kumchezea rafu Kichuya.

Kipa wa Simba, Aishi Manula, alifanya kazi ya ziada katika dakika ya 18, baada ya kupangua shuti la Hussein Seleman, aliyejaribu kuipangua ngome ya Simba kabla ya kuachia mkwaju huo.

Katika dakika ya 21, Rajesh Kotecha, alilimwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu Jonas Mkude.

Hali ilikuwa mabaya kwa Simba katika dakika ya 24, baada ya Manula kuonyeshwa kadi ya njano, kutokana na kumchezea rafu Pastory katika eneo la hatari aliyekuwa akielekea kufunga na mwamuzi kuamuru ipigwe penalti.

Penalti hiyo ilifungwa katika dakika ya 26 na Said Said na Mbao kuongoza kwa bao hilo.

Kuingia kwa bao hilo, kuliwaumiza wachezaji wa Simba ambao walielekeza mashambulizi langoni mwa Mbao, huku katika dakika ya 32, Kichuya alipoteza nafasi ya wazi ya kuifungia timu yake bao baada ya kupokea pasi ya Mohamed Ibrahim na kuachia shuti lililopaa juu ya lango la Mbao.

Dakika ya 42, kipa wa Mbao, Hasheem Mussa, alifanya kazi ya ziada baada ya kupangua shuti la Pascal Wawa, aliyekuwa akiunganisha krosi ya Clotus Chama na kuzaa kona ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Mbao kuongoza kwa bao moja.

Kipindi cha pili kilianza kwa Mbao kuliandama lango la Simba katika dakika ya 54, baada ya Said kujaribu kuipenya ngombe ya Simba na kufumua shuti lililotua mikononi mwa Manula.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems, katika dakika ya 54, alifanya mabadiliko kwenye kikosi chake kwa kumtoa Mohamed Ibrahim na kumwingiza Meddie Kagere.

Katika dakika ya 58, kocha Amri Said, alifanya mabadiliko kwa kumtoa Rajesh Kotecha na kumwingiza Evarigestus Mujwahuki.

Simba waliendelea kuliandama lango la Mbao, ambapo katika dakika ya 67, Kagere alishindwa kuisawazishia Simba baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa na Kichuya na mpira kutoka nje la lango la Mbao.

Simba ilifanya tena mabadiliko katika dakika ya 74, kwa kumtoa Kichuya na nafasi yake kuchukuliwa na Rashid Juma.

Mbao nao walifanya mabadiliko katika dakika ya 76, kwa kumtoa Hussein Seleman na kumwingiza Roland Msonjo.

Katika dakika ya 82, Said, alipoteza nafasi kuiandikia timu yake bao la pili baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona na kutoka nje kidogo ya lango la Simba.

Simba walikosa bao katika dakika ya 86, baada ya Kagere kushindwa kutumia vema makosa ya beki wa Mbao ambaye alirudisha mpira mfupi kwa kipa wake, Kagere aliuwahi mpira huo na kuachia shuti lililokwenda nje.

Mbao walifanya mabadiliko tena katika dakika ya 86, kwa kumtoa Abubakari Mfaume na kuingia Hamim Abdul na hadi dakika tisini zinamalizika, timu hiyo ilitoka kifua mbele kwa ushindi wa bao 1-0.

Kwa matokeo hayo, Mbao inaongoza kwenye msimamo wa ligi hiyo kwa kuwa na pointi 10 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi tisa, sawa na JKT Tanzania ikiwa nafasi ya tatu huku Azam ikiwa nafasi ya nne kwa kuwa na pointi nane, wakati Simba ikiwa ya tano kwa kuwa na pointi saba.

Katika michezo mingine ya ligi hiyo, African Lyon iliifunga Singida United mabao 3-2, katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, wakati Tanzania Prisons ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Kagera Sugar, katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mbao: Hasheem Mussa, Vicent Philipo, Amos Charles, David Mwassa, Peter Mwangosi, Ally Mussa, Said Said, Hussein Seleman, Rajesh Kotecha, Pastory Athanas na Ababukari Mfaume.

Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkud, Shiza Kichuya, Clotus Chama, John Bocco, Emmanuel Okwi na Mohamed Ibrahim.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles