Familia yaingilia Ronaldo kuoneshwa kadi nyekundu

0
2063

TURIN, ITALIA

BAADA ya nyota wa soka duniani kutoka klabu ya Juventus, Cristiano Ronaldo kuoneshwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Valencia juzi, dada wa mchezaji huyo amekuja juu na kudai kuna mipango imetengenezwa kwa ajili ya kutaka kumwangamiza mchezaji huyo kwenye soka.

Mchezaji huyo alioneshwa kadi nyekundu katika dakika ya 29 ya mchezo baada ya kumshika nywele beki wa Valencia, Jeison Murillo, wakati mchezaji huyo ameanguka chini kutokana na kuchezewa vibaya na Ronaldo.

Ronaldo alifanya hivyo kwa kumlalamikia mchezaji huyo kuwa hakumfanyia kitu chochote kibaya, lakini mwamuzi alikwenda moja kwa moja na kumwonesha kadi nyekundu.

Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Ronaldo kuoneshwa kadi nyekundu katika michezo 154 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, pia hakufanikiwa kupata bao kwenye mchezo huo japokuwa Juventus walishinda mabao 2-0.

Hata hivyo, hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Ronaldo kushindwa kufunga bao katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa tangu alipofanya hivyo mwaka 2012.

“Hii ni aibu kwenye mchezo wa soka, lakini ninaamini haki atatendeka, naona kuna mipango ya kutaka kumwangamiza kaka yangu, ila hawataweza kwa uwezo wa Mungu,” aliandika dada wa Ronaldo, Katia Aveiro, kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mchezaji huyo anaweza kuukosa mchezo wa michuano hiyo dhidi ya klabu yake ya zamani Manchester United kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Sheria ya kadi nyekundu ya moja kwa moja inaweza kumfanya mchezaji akose michezo mitatu kutokana na ukubwa wa kosa alilopewa kadi hiyo kwa mujibu wa Uefa, lakini kanuni za Uefa namba 50.01 zinazosimamia michuano hiyo zinasema iwapo kosa litakuwa kubwa sana, jopo la Uefa linaloangazia udhibiti, maadili na nidhamu lina haki ya kuongeza adhabu hiyo.

Ronaldo bila shaka ataikosa mechi itakayofuataa dhidi ya Young Boys, Oktoba 2, iwapo adhabu itaongezwa na kuwa mechi mbili, basi ataikosa mechi dhidi ya klabu yake ya zamani, Manchester United, Oktoba 23.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here