LIGI Kuu ya Tanzania Bara inatarajia kuendelea leo katika viwanja tofauti, huku timu ya Simba ikiwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuikaribisha timu ya Majimaji ya Songea.
Simba wanaingia katika uwanja huo wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kupata ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya Majimaji, kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza na baadaye katika mzunguko wa pili kupata suluhu katika mechi ya marudiano mjini Songea, katika msimu uliopita.
Licha ya kumbukumbu hiyo nzuri kwa Simba, lakini wanahitaji ushindi ili kuendelea kukalia usukani wa ligi hiyo wakiwa na pointi 13, baada ya kucheza mechi tano, huku wakisubiri kuvaana na watani wao, timu ya Yanga Oktoba Mosi.
Mechi nyingine zitakazochezwa leo, Ndanda wataikaribisha Azam FC katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mkoani Mtwara.
Azam, iliyo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 10, wanaingia uwanjani wakiwa na machungu ya kufungwa bao 1-0 na Simba katika mechi yao iliyopita.
Mechi nyingine itakuwa katika Uwanja wa Mabatini, Â Mlandizi, mkoani Pwani, JKT Ruvu itakapoikaribisha Mbeya City, huku Tanzania Prisons wakiwakaribisha Mwadui FC katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, wakati Mtibwa Sugar watakuwa katika Uwanja wa Manungu, Morogoro, kucheza na Mbao FC.
Ligi hiyo itaendelea kesho ambapo timu ya Stand United itawakaribisha mabingwa watetezi wa ligi hiyo, timu ya Yanga.
Mechi nyingine itazikutanisha Ruvu Shooting na Toto African katika Uwanja wa Mabatini, mkoani Pwani, wakati African Lyon itaikaribisha Kagera Sugar katika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.