Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wanachama na mashabiki wa Klabu ya Simba katika Kata ya Kivule wamezindua tawi lao huku wakitamba kufanya makubwa zaidi.
Uzinduzi huo ulipambwa kwa maandamano yaliyoanzia eneo la Banana hadi Kivule huku wakionyesha vikombe vitatu ambavyo Klabu ya Simba imevinyakua mwaka huu vya Klabu Bingwa, FA na Simba Queens.
Mwenyekiti wa tawi hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kivule, Amos Hanganya, amesema lilianzishwa Januari mwaka huu na mpaka sasa lina wanachama 75 na mashabiki 400 huku wakiwa na mkakati wa kuongeza wanachama zaidi.
“Tuna malengo ya muda mrefu ya kujenga ofisi ya kudumu, kufungua duka la jezi, kuongeza wanachama, kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii kwa makundi mbalimbali na kusaidiana kwa kuinuana kiuchumi,” amesema Hangaya.
Naye mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Wanachama na Mashabiki, Hamisi Kisiwa, amewataka wanachama na mashabiki wa tawi hilo kuendelea kuwa na umoja na kushirikiana ili klabu hiyo izidi kufanya vizuri zaidi.
“Nawapongeza kwa kufungua tawi kwa sababu tunajua wanachama na mashabiki wana mchango mkubwa katika timu, wachezaji peke yao hawawezi kushinda bila kuwepo na hamasa yenu,” amesema Kisiwa.
Kwa upande wake Msimamizi wa Kivule Garden Park, Anna Kiondo, amesema wametoa kiwanja ili kuliwezesha tawi hilo kujenga ofisi ya kudumu na kufanya uwekezaji mwingine.
Amesema pia wanaendelea kuboresha huduma zao na kwamba wako kwenye mchakato wa kujenga bwawa la kuogelea na kuwashauri wakazi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji kwenda kupata huduma.
Katika uzinduzi huo mgeni rasmi pia amewakabidhi kadi za uanachama wanachama wapya wa klabu hiyo na kulitaka tawi hilo kuongeza wanachama zaidi.