26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Simba kasi ile ile

Pg 32*Yalipiza kisasi kwa Prisons, Kagera yaua, Majimaji safi

NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

VINARA wa michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba jana waliendeleza kasi yao ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo baada ya kuchomoza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Bao pekee la ushindi lililowapa Simba pointi tatu muhimu na kufikisha pointi 54 na kuzidi kuwaacha mahasimu wao, Yanga lilipachikwa wavuni ni Awadhi Juma dakika za lala salama.

Kwa matokeo ya jana, Simba ilizidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kujikusanyia pointi 54 baada ya kushuka dimbani mara 23 wakifuatiwa na Yanga wenye pointi 50 lakini wakiwa na michezo miwili mkononi huku Azam wakishika nafasi ya tatu kwa pointi 47.

Wekundu hao wa Msimbazi wamelipiza kisasi kwa maafande wa Prisons ambao katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi waliwapa kipigo cha bao 1-0 wakicheza nyumbani katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya wakati huo kikosi cha Simba kikinolewa na kocha Mwingereza, Dylan Kerr.

Katika mchezo wa jana ambao ulichezeshwa na mwamuzi, Jacob Adongo kutoka Mara, wenyeji Simba walijitahidi kutengeneza nafasi 10 za kufunga dakika 45 za kipindi cha kwanza lakini walishindwa kupata bao kutokana na tatizo la umaliziaji.

Maafande wa Prisons walitengeneza nafasi ya kufunga bao dakika ya 11 lakini shuti lililopigwa na Jeremia Juma lilidakwa kirahisi na kipa wa Simba, Vicent Angban.

Simba walijibu mapigo dakika ya 13 kupitia kwa mshambuliaji, Hamis Kiiza, aliyepenyezewa pasi safi na beki wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, lakini akashindwa kuitumia vyema nafasi hiyo kabla ya beki, Hassan Ramadhan ‘Kessy’ kukosa bao la wazi dakika ya 18 baada ya kuwatoka mabeki na kupiga shuti lililopaa juu ya lango.

Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa hazijafungana, ambapo kipindi cha pili kilianza kwa Prisons kufanya shambulizi kali dakika ya 47 kupitia kwa Benjamini Asukile ambaye alipiga shuti lakini likagonga mwamba.

Simba nao waliendeleza kasi baada ya kurejea uwanjani ambapo dakika ya 51, Ibrahim Ajib, alipiga shuti la mbali lililogonga mwamba baada ya kupewa pasi safi na Tshabalala na dakika ya 54 alipiga shuti lililopanguliwa na kipa, Ben Kakolanya wa Prisons na kuwa kona.

Awadhi aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Justice Majabvi ndiye shujaa wa Simba aliyeifungia bao la ushindi dakika ya 86 baada ya kupiga shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni.

Simba: Vicent Angban, Jjuuko Murshid, Novaty Lufungo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Ramadhan Hassan ‘Kessy’, Justice Majabvi/Awadhi Juma, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Mussa Hassan ‘Mgosi’/Danny Lyanga, Ibrahim Ajib na Hamis Kiiza/Paul Kiongera.

Prisons: Ben Kakolanya, Salum Kimenya, James Mwasote, Lugano Mwangama, Laurian Mpalile, Jumanne Elfadhil, Lambarti Sabiyanka, Juma Seif/Fred Chudu, Mohamed Mkopi, Jeremia Juma/ Meshack Selemani, na Benjamin Asukile.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Mgambo Shooting ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Mwadui FC wakicheza nyumbani katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Bao la Mwadui lilifungwa na Morris Kaniki dakika ya 13 kipindi cha kwanza kabla ya Fuly Maganga wa Mgambo Shooting kusawazisha katika dakika ya 76.

Kagera Sugar wakicheza katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga walitoa kipigo kikali kwa Coastal Union baada ya kuwachapa mabao 3-0 yaliyofungwa na Mbaraka Yussuf aliyepiga ‘hat trick’ yake ya kwanza Ligi Kuu Bara.

Kwa upande wao Majimaji walicharuka katika uwanja wao wa nyumbani wa Majimaji, Songea na kuichapa Stand United ya Shinyanga bao 1-0, lililofungwa na Lulanga Mapunga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles