24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA   ILIVYOJIPANGA KUSHANGAZA ‘SIMBA DAY’

NA SOSTHENES NYONI – DAR ES SALAAM


UMEKUWA utamaduni wa kawaida kila ifikapo Agosti 8, Klabu ya Simba husherehekea siku yake inayofahamika kama ‘Simba Day’.

Klabu ya Simba hutumia siku hii kutambulisha kikosi chake kitakachoshiriki msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Utaratibu ambao umekuwa ukitumiwa na klabu hii ni kutambulisha mchezaji mmoja mmoja na namba ya jezi atakayoitumia.

Kwa mwaka huu, pia Klabu ya Simba imepanga kuadhimisha siku hii itakapofika Agosti 8.

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah, maarufu kama Try Again, anasema tofauti na miaka iliyopita, safari hii wamejipanga kuhakikisha tamasha hili linakuwa na sura tofauti na ile iliyozoeleka.

“Nawaomba mashabiki, wanachama na wapenzi wa Simba nchi nzima wajitokeze kwa wingi Siku ya Simba Day.

“Kimsingi tumejipanga kuja kivingine safari hii kwa kuhakikisha kila atakayehudhuria anabaki na burudani ya kudumu moyoni mwake,” alisema Abdallah.

Abdallah anasema kabla ya kufikia kilele na siku ya klabu hiyo, yaani Agosti 8, zitatanguliwa shughuli tofauti, ambazo zimepangwa kuanza leo.

Anazitaja shughuli hizo kuwa ni pamoja na kufanya usafi, uzinduzi wa jezi mpya za klabu hiyo na ziara ya kuwatembelea maveterani wa timu hiyo na watani wao wa jadi, Yanga na kutembelea vituo vya watoto yatima kwa lengo la kuwafariji.

Anasema shughuli za usafi zinatarajiwa kufanywa na matawi ya klabu hiyo, hasa wakilenga maeneo ya kijamii.

Abdallah anasema zoezi la uzinduzi wa jezi wamepanga kulifanya kesho, sambamba na kuanza kuuzwa kwa mashabiki wa klabu hiyo.

“Lengo letu ni kuuza jezi 10,000 kwa wapenzi, wanachama na mashabiki wa Simba,” anasema Abdallah na kuongeza:

“Utaratibu wa wapi zinapatikana tutauweka wazi, muhimu tunawaomba mashabiki wetu wanunue jezi halisi ili kuichangia klabu yao.”

Anasema shughuli ya kutembelea watoto yatima itahusisha wachezaji wa klabu hiyo kwa kushirikiana na taasisi ya Mo Foundation.

Burudani ya kutosha

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Haji Manara, anasema mbali ya kushuhudia pambano la soka kati ya Wekundu hao na Asante Kotoko ya Ghana, pia wamejipanga kuwapa burudani ya muziki mashabiki watakaohudhuria kilele cha tamasha lao.

Anawataja wasanii watakaotumbuiza siku hiyo kuwa ni Tunda Man, Mwasiti, Msagasumu na Nandi kwa upande wa muziki wa Bongo Fleva, wakati JB na Monalisa wanawakilisha wasanii wa filamu.

Historia ya Simba Day

Tamasha la siku ya Klabu ya Simba lilianzishwa rasmi mwaka 2009, wakati miamba hiyo ya Msimbazi ikiwa chini ya uongozi wa Hassani Dalali, ambaye alikuwa mwenyekiti na Katibu Mkuu wake, Mwina Kaduguda.

Yafuatayo ni matokeo ya Simba tangu tamasha la Simba Day lilipoanzishwa.

Simba 1-0 SC Villa, Uganda (2009)

Hii ilikuwa mechi ya kwanza tangu kuanzishwa kwa tamasha hilo.

Mchezo huo ulichezwa Uwanja wa Uhuru (zamani Taifa), huku mfungaji wa bao pekee la Simba akiwa Mkenya, Hilary Echessa.

Simba 0-0 Express, Uganda (2010)

Kwa mara nyingine Simba ilialika timu kutoka Uganda kwaajili ya kucheza nayo mchezo maalumu wa kirafiki wa tamasha lake.

Lakini safari hii, Simba ilishuhudiwa ikishindwa kuwafurahisha mashabiki wake baada ya kulazimishwa suluhu na Express.

Simba 0-1 Victors, Uganda (2011)

Tamasha hili lilifanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, ulioko jijini Arusha.

Kilichoshuhudiwa siku hiyo ni Simba kupoteza mbele ya wageni wao baada ya kuchapwa bao 1-0.

Bao la wageni siku hiyo lilifungwa dakika ya 70 kwa mkwaju wa penalti wa Patrick Sembuya.

Simba 1-3 Nairobi City Stars, Kenya (2012)

Mambo hayakuwa mazuri kwa mara nyingine  katika tamasha la mwaka huo, baada ya kukutana na kipigo cha mabao 3-1.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, mabao ya Nairobi City Stars yalifungwa na Duncan Owiti, Bruno Okullu na Boniface Onyango. Bao pekee la Simba lilifungwa na Felix Sunzu dakika ya 15.

Simba 4-1 SC Villa, Uganda (2013)

Wekundu wa Msimbazi, Simba, walirejea Uganda na kuumana na SC Villa na kuendelea kuitambia kwa mara nyingine.

Katika mchezo huo, uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, mabao ya Simba yalifungwa na Jonas Mkude, William Lucian ‘Gallas’ na Betram Mwombeki aliyefunga mawili.

Simba 0-3 Zesco, Zambia (2014)

Mwaka huo nao haukuwa mzuri sana kwa Simba, baada ya kushuhudiwa ikipoteza kwa kuchapwa mabao 3-0 na miamba ya Zambia, timu ya Zesco.

Mabao ya Zesco katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, yalifungwa na Jackson Mwanza, Clatos Chane na Mayban Mwamba.

Hiki kilikuwa kipigo cha tatu Simba kukutana nacho tangu ilipoanza kuadhimisha siku yake.

Simba 1-0 SC Villa, Uganda (2015)

Timu ya Villa iliendelea kuwa mnyonge kwani katika tamasha la mwaka huu,  ilikutana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Wekundu hao.

Bao pekee la Simba siku hiyo lilifungwa na kiungo Awadh Juma.

Simba 4-0 AFC Leopard, Kenya (2016)

Tamasha jingine la Simba Day ni lile lililofanyika mwaka 2016.

Vigogo wa Kenya, AFC, ndio walipata mwaliko wa kuumana na Simba, lakini walikutana na kipigo kikali cha mabao 4-0.

Mshambuliaji  Ibrahim Ajib, ambaye kwa sasa anaichezea Yanga, alifunga mawili, mengine yakipachikwa wavuni na Laudit Mavugo na Shiza Kichuya.

Simba 1-0 Rayon Sports, Rwanda (2017)

Mohamed Ibrahim alikuwa shujaa wa Simba siku hiyo, baada ya kuifungia bao pekee dhidi ya Rayon Sports.

Sijui nini kitatokea katika tamasha la mwaka huu, ambalo litakuwa la tisa kwa Klabu ya Simba, tusubiri tuone.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles