27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA BADO WANAKIBARUA KIZITO KUCHUKUA UBINGWA   

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM


TIMU ya Simba bado ina kabiliwa na kibarua kigumu kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, licha ya  kuongoza msimamo wa ligi.

Ligi hiyo imebakisha michezo miwili ili kuingia mzunguko wa pili ambao utakuwa wa lala salama.

Simba,  wamefanikiwa kuwa kileleni baada ya Azam FC ambao walikuwa wakifungana pointi, kushindwa kuwafunga Majimaji na kushuka hadi nafasi ya pili wakiwa na pointi 27.

Azam FC, wangeweza kuibana Simba, kwenye uongozi wa ligi endapo wangeshinda mchezo huo, lakini sare waliyoipata iliwafanya kufikisha pointi 27 na kuwaacha Simba wakiongoza kwa pointi 29, baada ya kucheza michezo 13 huku mabingwa watetezi Yanga wakisalia kwenye nafasi ya tano na pointi zao 22.

Yanga pamoja na kushika nafasi ya tano na kuwa nyuma kwa pointi saba dhidi ya vinara Simba na pointi nne  kwa Azam FC,  lakini nao kikosi chao bado kimeonyesha mapungufu na kocha George Lwandamina, anatakiwa kujipanga vyema mzunguko wa pili ili kurudi kwa kasi na kuweza kutetea taji lao.

Kikosi cha Simba awali kilionekana kusuasua ingawa ilikuwa ikiongoza ligi kwa tofauti ya mabao, mashabiki wengi wa timu hiyo walionyesha kutofurahia mwenendo wa timu yao.

Simba ilionyesha mapungufu makubwa kwenye safu yake ya ushambuliaji, licha ya kuundwa na wachezaji wenye majina makubwa, lakini walishindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo, huku wakijikuta wanapata ushindi kiduchu wa bao 1-0.

Mwenendo huo mbaya wa timu ulimweka katika wakati mgumu kocha Joseph Omog, kwani pamoja na jitihada alizozifanya aliishia kutimuliwa.

Nafasi yake sasa imeweza kuchukuliwa na Mfaransa Pierre Lechantre.

Hata hivyo kocha msaidizi wa Simba Masud Djuma, ambaye alikuwa akikaimu nafasi hiyo, hivi karibuni ameweka wazi kuwa mwenendo wa timu hiyo si mzuri na wachezaji wanapaswa kubadilika.

Mabadiliko ya mfumo pamoja na uvivu kwa wachezaji, vimekuwa vitu ambavyo wakati mwingine vinarudisha nyuma mapambano ya timu hiyo kuelekea ubingwa msimu huu.

Lakini kwa upande mwingine kinachowauma mashabiki pamoja na baadhi ya viongozi wa timu hiyo ni kiasi cha fedha ambazo zimetumika kufanya usajili wa Bilioni 1.3,  ambazo hazijaonyesha tofauti yoyote na kile kikosi cha Azam kinachoshika nafasi ya pili, huku kikiwa na idadi kubwa ya wachezaji chipukizi wasio na majina.

Kiujumla ligi ya msimu huu, imekuwa na ushindani mkubwa ikilinganishwa na  misimu iliyopita, hivyo kuna kazi kubwa kwa Simba,Yanga pamoja na Azam ambazo zimeshawahi kuonja ladha ya ubingwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles