Na OSCAR ASSENGA-ARUSHA
SIMBA aliyefanyiwa upasuaji tumboni eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, amemaliza muda wa uangalizi wa madaktari bingwa.
Kinachosubiriwa sasa ni Serikali kuruhusu wapi na sehemu gani awekwe mnyama huyo kwa maisha yake ya baadaye.
Hayo yalisemwa juzi na mwangalizi wa simba huyo, Dk. Athanas Mnyaki wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea hifadhi hiyo.
Alisema baada ya kumalizika upasuaji na uangalizi maalumu wa simba huyo, wataalamu walimrejesha kwenye hifadhi hiyo, lakini licha ya mama yake kumpokea, shangazi yake alimkataa na kuanza kumshambulia.
Dk. Mnyaki alisema kuwa ni desturi ya wanyama hao kuishi kwa ukoo, lakini inapotokea mmoja wao kuwa nje ya familia husika kwa zaidi ya siku mbili, humkataa kwa kumpiga na wakati mwingine hata kumuua anaporejea.
Alieleza kuwa kutokana na jitihada za kumrejesha simba huyo katika hifadhi ya Ngorongoro  kushindikana, inasubiriwa kauli ya Serikali ya
wapi au nini kifanyike kwa maisha yake.
Kuhusu matatizo yaliyokuwa yakimkabili simba huyo, Dk. Mnyaki alisema kuwa alikuwa
akikabiliwa na udhaifu wa misuli ya nyama za tumbo na kusababisha kuwa kubwa kiasi cha kukaribia kugusa chini.
Tatizo hilo licha ya kumpunguzia uwezo wake wa uwindaji, lakini pia ungehatarisha maisha yake kwa kushindwa kukamata wanyama na hivyo kukosa lishe.