27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Silaha 473 za uhalifu na risasi 328 zakamatwa Tabora

Na Allan Vicent, Tabora

Jeshi la Polisi mkoani Tabora kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) kupitia Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Magharibi (KDU-TABORA) na Pori la Akiba Ugalla wamekamata jumla ya silaha 473 na risasi 328 zilizokuwa zikitumika katika matukio mbalimbali ya kihalifu.

Hayo yamebainishwa jana na Kamanda wa Polisi mkoani hapa ACP Safia Jongo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake.

Alisema silaha hizo zimekamatwa kutokana na oparesheni ya pamoja ambayo imeendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali mkoani hapa ikiwemo kwenye mapori ya hifadhi.

Alitaja silaha zilizokamatwa kuwa ni AK 47/SMG  (12),  G3 (2), Shortgun (29), Riffle (23) na Magobore 407 ikiwemo risasi za AK 47 (134), G3 (28), Shortgun 45 (22), Honet 8, Pistol 25 na za kienyeji 88, zote zinatarajiwa kupelekwa Makao Makuu ya Polisi kwa ajili ya kutekelezwa.

 Aidha katika oparesheni hiyo yalikamatwa magari 2 yenye namba T 502 BMJ, na T 451 AMB aina ya Cresta ambayo yalikuwa yanatumika katika matukio ya uhalifu wa aina mbalimbali ndani na nje ya Mkoa huo huku akibainisha kuwa wanawasaka wamiliki halali wa magari hayo.

Kamanda Safia aliongeza kuwa kutokana na oparesheni inayoendelea katika Mkoa huo wamefanikiwa kukamata watuhumiwa 34 ambao wamekuwa wakijihusisha na matukio ya mauaji ya kutumia silaha za jadi huku akifafanua kuwa matukio ya aina hiyo yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Aidha, aliongeza kuwa watu 3 (majina yao yamehifadhiwa) wamekamatwa wilayani Sikonge wakiwa na silaha aina ya AK 47 maarufu kama SMG 1, Short gun 1 na magobore 2 zilizokuwa zimefichwa ndani ya bani na watu wengine 3 wamekamatwa na silaha katika mapango ya mlima wa Ichemba wilayani Kaliua.

Safia alibainisha kuwa pia wamemkamata Ramadhan Mkenda (62) mkazi wa Kaliua akiwa na mitambo ya kutengeneza silaha za kienyeji aina ya shortgun, gobore na vipuri vya kutengeneza silaha hizo.

Aliongeza kuwa pia wamekamata mtu 1 akiwa na silaha aina ya shortgun yenye no.36414, risasi zake 4 na maganda 53 huko katika kitongoji cha Kaselya kijiji cha Igalali kata ya Kitangili wilayani Nzega.

Aidha gobore 20, pistol za kienyeji 10 na jumla ya watuhumiwa wa ujambazi 25 walikamatwa.

Ili kukomesha matukio ya uhalifu na wahalifu katika mkoa huo aliwataka alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi hilo kwa kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu na wahalifu ili wahusika wote wakamatwe na kuchukuliwa hatua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles