29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

SIKU YA TANZANIA  2018, YAANZA KUSHIKA KASI DALLAS, TEXAS

Na, SARAH MOSSI, aliyekuwa Zanzibar


APRILI, mwaka huu, Jumuiya ya Watanzania waishio Dallas, Texas watakuwa na siku maalumu inayoitwa ‘Siku ya Tanzania’ Siku hii ni maalumu kwa Wanajumuiya hao kukutana na kubadilishana mawazo, kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, kuwaeleza wawekezaji juu ya hali nzuri ya uwekezaji nchini Tanzania pamoja na kutafakari Utanzania wao. Lakini pia siku hii huchagizwa na burudani mbalimbali za wasanii kutoka Tanzania, burudani za watoto wa Kitanzania na baadaye shughuli mbalimbali zinazofanana na siku hiyo.

Hata hivyo katika mahojiano maalumu na Mwandishi wa gazeti hili kuhusiana na siku hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania, Dallas, Texas, Ben Kazora alisema wamepanga kumwalika kiongozi wa ngazi ya juu wa Serikali kuwa mgeni rasmi kwenye shughuli hiyo ambayo alisema kwao wao wanaithamini kwa vile ndio wakati wao mwafaka wa kujivunia Utanzania wao baada ya kuishi Ughaibuni kwa kipindi kirefu.

Kazora alisema kama itampendeza wamepanga kumwalika Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi na tayari taratibu za kupeleka mwaliko huo kwa Serikali kupitia  Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje zimeanza.

Hivi karibuni Mwandishi wa makala haya alipata nafasi ya kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais, Samia Suluhu nyumbani kwake, Tunguu Zanzibar na  moja kati ya maswali aliyomuuliza iwapo itampendeza kupokea taarifa hiyo ya mwaliko na alikuwa na haya ya kusema:

“Nikipata nafasi kama hiyo ni kuwaambia tu mabadiliko ambayo sasa Tanzania yanatokea ni kwamba wawekezaji wengi wao walikuwa wakivunjika moyo wakija Tanzania kwa mambo ya rushwa lakini pia ucheleweshaji, Mwekezaji anataka akija hapa Januari ikifika Februari anataka awe ameshajua anawekeza wapi terms of conditions ni zipi, mambo ya kodi ni yepi na main power ni zipi awe ameshajua na awekeze,”

Samia alisema mwekezaji anapozungushwa kwa  miaka miwili anakuwa disappointed anaondoka na kusisitiza wawekezaji wengi wameondoka wamekwenda nchi jirani ambao wamebadilisha sera zao na wako vizuri.

“Kwahiyo sisi sasa kwenye hii sera mpya ya uwekezaji ambayo inasema mazingira mapya ya kufanyia kazi mambo mengi yatakuwa yamebadilika na nitakwenda na kitabu kitakachoelezea kwamba sasa tunabadilisha mazingira ya kufanyia biashara na sasa conditions ni moja, mbili, tatu, nne tano, tumetoka kutoka siku hizo na sasa tuko siku hizi, tumetoka kwenye kodi hizo na sasa tuko kwenye kodi hizi,” alisema Makamu wa Rais.

Akizungumzia  suala la utendaji serikalini, Samia alisema wananchi  ni mashahidi kwamba sasa nidhamu ya watendaji serikalini imeongezeka maradufu na sio nidhamu ya woga kama ambavyo baadhi ya ya watu wanavyoponda.

“Hata kama ni nidhamu ya woga lakini mageuzi yapo. Sasa hivi unakwenda serikalini unasikilizwa na kuhudumiwa kwa muda mfupi na kwa hiyo tumebadilisha system ya kufanya kazi serikalini,” alisisitiza.

Akizungumzia uwekezaji kwenye bandari za Tanzania pamoja na viwanja vya ndege, Samia alisema uwekezaji unategemea bandari pia na viwanja vya ndege na kusisitiza yapo mabadiliko makubwa kwenye bandari za Tanzania na viwanja vya ndege ili kumrahisishia mwekezaji kusafirisha mizigo yake kwa haraka na kutumia muda mchache.

”Lakini uwekezaji unategemea bandari pia na viwanja vya ndege vyetu na kama mnavyoona mabadiliko makubwa yapo kwenye bandari zetu na viwanja vya ndege vyetu, lakini pia uwekezaji pia ni miundombinu ya usafirishaji. Tunajenga Reli ya Kati ambayo itakwenda kwa haraka zaidi, itapeleka mizigo kwa siku chache zaidi, mingi zaidi na kutumia spidi ndogo zaidi. Na uwekezaji ni soko, anayewekeza hapa anategemeea soko la nchi tisa zilizotuzunguka lakini hata nje ya hapo. Sasa ukiwawekea miundombinu rahisi ya kusafirisha bidhaa zao mwekezaji anavutika,” alisema

“Lakini pia tunayo TAZARA ambayo sasa hivi iko kwenye mazungumzo, barabara tunajenga na madaraja tunajenda kwahiyo tunayo mabadiliko makubwa ambayo yalianza Awamu ya Nne na lazima tuseme ukweli tulianza huko nyuma sisi tunayachukua na tunayapeleka kwa kasi ili kubadilisha hali ya uwekezaji nchini. Kwahiyo tuna mengi ya kuwaambia wawekezaji kuwavuta waje kwetu

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania, Dallas, Texas, Ben Kazora alisema tofauti kati ya Siku ya Tanzania 2017 na Siku ya Tanzania 2018, itaonekana wazi kwani mwaka 20017 ulikuwa wa uzinduzi wa Siku hiyo na kulikuwa na matukio ya kufurahisha ikiwamo usimikaji wa bendera ya Tanzania katika ukumbi wa moja ya majiji makubwa kabisa nchini Marekani-Dallas.

“Hili ni jiji la nne kwa ukubwa wa Pato la Ndani (GDP) nchini Marekani na pia miongoni mwa majiji 10 yanayoongoza kwa wingi wa watu nchini humu,” alisema Kazora.

Kazora alisema kusimikwa kwa bendera ya Taifa la Tanzania kumeonesha kukubalika kuzaa matunda kwa Tanzania hasa linapokuja suala la ongezeko la idadi ya watalii na wawekezaji  vitega uchumi.

 

Mwenyekiti huyo alisema Mwaka 2017 walikuwa  na njia za ubunifu ikiwamo kuhusisha familia na kuwapo kwa shughuli za watoto katika Tamasha hilo la Siku ya Tanzania. Aidha  tamasha hilo liliruhusu wafanyabiashara kutoka Tanzania kuonesha bidhaa na huduma zao.

“Yote hayo yalitokea wa kutoza kiwango kidogo cha ada kwa washiriki.” Alisisitiza Kazora.

Hata hivyo, Kazora alisema mwaka 2018 unakuja na vitu vipya ikiwa ni pamoja na tamasha hilo kuwa bure kwa kila mtu na hivyo matarajio yao ni kupata washiriki wengi wa  Wamarekani ambao wataweza kujifunza kuhusu Tanzania huku wakinunua bidhaa za Tanzanian ambazo zitauzwa na wafanyabiashara.

“Ni kwa sababu hii, tunawakaribisha Watanzania wenye bidhaa na huduma kuja mjini Dallas kwa ajili ya biashara,” alisisitiza.

Kazora alisema Siku ya Tanzania 2018 itakuwa pia tofauti na iliyopita kwani itahusisha uendeshaji wa mikutano ya kibiashara baina ya viongozi wa kibiashara wa Tanzania na Marekani pamoja na kuanzisha ushirikiano mpya na  kuruhusu mahusiano ya kina baina ya Tanzania na Marekani.

Alisema Siku ya Tanzania 2018 wameandaa  michuano ya soka na mpira wa kikapu ambapo jamii zitaonesha uwezo wao na kuongeza tayari wameialika Timu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatarajiwa kuoneshana umwamba na  Watanzania waishio Marekani.

“Hii itakuwa mara ya kwanza kwa wabunge wa Tanzania kujishughulisha na Watanzania waishio nje katika tukio la kijamii la kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na watu wake waishio nje yaani  Diaspora.

Kwa mujibu wa Kazora Aprili 29, 2018 kutakuwa na shindano la kuendesha baiskeli la kilometa tano ili kuchangisha fedha kwa ajili ya kuinua mwamko juu ya  Saratani ya kizazi ambayo imewaathiri sana wanawake wa Tanzania na kuongeza mapato ya  shughuli hiyo yatakwenda kununulia chanjo na misaada mingine nchini Tanzania.

Akizungumzia kuhusiana na kauli mbiu ya Siku ya Tanzania, 2018, alisema  itachagizwa na Mlima Kilimanjaro, ambao ndio mlima mrefu barani Afrika pamoja na dhamira ya Taifa ya kuwa eneo linaloongoza kwa wingi wa watalii barani Afrika ikiwa ni pamoja na ukuaji wa kasi wa uchumi.

“Ni kwa sababu hiyo, kauli mbiu yetu kwa Siku ya Tanzania 2018 ni: Safari kuelekea Juu., kupanda kuelekea vilele vipya.

Alisema Mwaka huu pia wamekaribisha wageni kutoka mabara yote ikiwamo  Norway hadi Dubai, Uganda hadi Australiana kusisitiza wanaamini juhudi hizo ni kwa ajili ya Diaspora wote wa Tanzania.

Alisema maandalizi ya Siku ya Tanzania 2018 yalianza Mei 2017na  kuviomba vyombo vya habari Tanzania kushirikiana nao katika juhudi hizo.

“Juhudi kama hizo pia zimehusisha vyombo vya habari vya Marekani.  Tumeshajenga ushirikiano na vituo vya redio na televisheni vya Marekani,”alisema.

Ili kuhakikisha viongozi wa kibiashara kutoka Tanzania kunufaika zaidi, Kazora alisema  wamekaribisha viongozi wa kibiashara kueleza mahitaji yao ya kibiashara mapema ili waweze kuandaa mikutano ya kibiashara wakati wa ziara yao.

“Mwaka  2018 tumekuja na ubunifu wa kimkakati unaotutambulisha kupitia namba maalumu (+ 1 817 50 TZ USA). Namba hii imelenga kututambulisha sambamba na rasilimali nyingine mpya, wavuti yetu: (www.tanzaniaday.com). Juhudi hizi za kukuza jina la Tanzania nchini Marekani ni mkakati wa kipindi kirefu na tunapenda kutoa mwito kwa Watanzania wote kuungana na juhudi hizi,

Majirani zetu wa Kaskazini wamefanya kazi nzuri ya kujitangaza sana na hii imeshuhudia idadi kubwa ya watalii na sasa wameanzisha safari za moja kwa moja kutoka Marekani. Tanzania ni mahali stahili pa kumiliki fursa hizi na kuwa mbele ya majirani zake zote,

“Sisi Watanzania tuishio ng’ambo tunayo imani kuwa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dk. John. P. Magufuli ataunga mkono juhudi za Siku ya Tanzania 2018 wakati tukiendelea kupeperusha bendera ya Tanzania nchini Marekani kwa ufahari na kuendeleza ajenda zake., “ alisisitiza.

Kwa mujibu wa Kazora ni Watanzania pekee waishio ng’ambo ndio wataweza  kuisimulia Tanzania vizuri na kwa kina katika nchi hizi za kigeni ambazo zimekuwa nyumbani namba mbili kwao baada ya Tanzania.

Kazora pia alitoa mawasiliano maalumu kwa Watanzania waishio ndani na  nje ya Marekani watakaopenda kushiriki siku hiyo kwa ajili ya kupata taarifa mbalimbali ambayo ni  email. [email protected].

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles