24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

ALIYEJIUNGANISHIA BOMBA LA MAFUTA APANDISHWA KORTINI

Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM


MFANYAKAZI Mstaafu wa Bomba Kuu la Mafuta la Tanzania na Zambia (TAZAMA), Samweli Nyakirang’ani anayedaiwa kutoboa bomba kuu la mafuta ya dizeli na kujiunganishia hadi nyumbani kwake amefikishwa mahakamani kwa uhujumu uchumi.

Mshtakiwa huyo, mkewe Nyangi Mataro na wenzao watano walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na kusomewa mashtaka matatu chini ya sheria ya uhujumu uchumi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Wakili wa Serikali Mkuu, Peter maugo  akisoma mashtaka aliwataja washtakiwa kuwa ni Samweli (63), Nyangi (54) Mwalimu wa Shule ya Msingi Ufukoni, Farijia Ahmed( 39) mfanyabiashara, Malaki Mathias(39) mfanyabiashara, Kristomsi Angelusi (25) mfanyabiashara, Pamfilis Nkoronko (40) fundi ujenzi na Herry Fredrick (38) mfanyabiashara.

Maugo alidai washtakiwa kwa pamoja wanashtakiwa kwa makosa matatu ya uhujumu uchumi, wanadaiwa kujiunganishia bomba kwenye bomba la mafuta isivyo halali kinyume cha sheria ya mafuta.

“Mheshimiwa washtakiwa kwa pamoja kati ya mwaka 2015 na Januari 8, mwaka huu maeneo ya Muungano, Tungi Kigamboni, jijini Dar es Salaam waliunganisha bomba la nchi moja lisiloshika kutu kwenye bomba lenye upana wa nchi 24 lenye mafuta ya dizeli bila kibali, mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania,

“Shtaka la pili, washtakiwa mnadaiwa katika kipindi hicho mliharibu miundombinu kwa kutoa bomba la nchi 24 mali ya mamlaka hiyo lililokuwa linatumika kusambaza mafuta ya dizeli.

“Katika shtaka la tatu, washtakiwa mnadaiwa kuharibu kifaa muhimu kinachotumika kusambaza mafuta, mlitoboa bomba la nchi 28 lililokuwa linatumika kusambaza mafuta ya dizeli mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania,” alidai Maugo.

Wakili Maugo alimaliza kuwasomea washtakiwa mashtaka yanayowakabili lakini hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Jamhuri ilidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, waliwasilisha hati ya kuzuia dhamana iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kwa washtakiwa wote.

Wakili Maugo alidai washtakiwa wanayo haki ya kuzungumzia uhalali na uwepo wa hiyo hati ya kuzuia dhamana. Aliomba kesi iahirishwe  hadi tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa hawakuzungumza chochote, Hakimu Simba aliamuru waende rumande hadi Januari 30 mwaka huu kesi yao itapotajwa.

Washtakiwa walikuwa wakishikiliwa na Jeshi la Polisi, ilidaiwa walilotoboa bomba la kwanza na kulikuta likiwa na mafuta ghafi wakaliziba kisha kutoboa lingine lililokuwa na dizeli na kuliunganisha hadi nyumbani kwa mshtakiwa wa kwanza.

Tukio hilo lilibainika baada ya mafuta yaliyokuwa yanavuja kuanza kusambaa barabarani. Januari 6, mwaka huu wataalamu walienda kuchimba ili kubaini tatizo la mafuta kusambaa barabarani, walipochimba walikuta mabomba matatu ya mafuta, mawili yakiwa yametobolewa na moja lililokuwa linapitisha mafuta ghafi likiwa limezibwa.

Inadaiwa mafuta yakishushwa kwenye meli hupita katika mabomba hayo yaliyopo jirani na nyumbani kwa mshtakiwa wa kwanza kwa kusukumwa na mashine kuelekea kituo cha kuhifadhia cha Tazama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles