Na MWANDISHI WETU-SIMIYU
WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amesema Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), litashirikiana na wananchi kutoa mafunzo ya uanzishwaji viwanda vidogo ili kufikia azma ya Serikali ya viwanda kwa vitendo.
Hayo aliyasema juzi katika ziara ya kukabidhi mkandarasi eneo la kujenga mtaa wa viwanda katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambapo Mwijage alifungua ofisi hiyo na kuwataka wananchi kutumia fursa ya kuwepo ofisi za SIDO mkoani humo kujipatia maarifa ya kuanzisha viwanda.
“Ili kufanya vizuri katika kuanzisha viwanda vidogo, lazima kupata elimu na tayari SIDO wapo mkoani Simiyu kutekeleza wajibu huo, nawaomba wananchi wajitokeze kupata mafunzo,” alisema Mwijage.
Alisema mpango wa Serikali kwa mwaka 2018/19 ni kuiwezesha SIDO kuwaongoza Watanzania kuanzisha viwanda vidogo na vya kati ili kutekeleza azma ya Serikali ya viwanda kwa vitendo.
“Simiyu ina fursa nyingi za uchumi, changamkieni fursa hizi hasa katika kuongeza thamani ya mazao ili kupata tija zaidi ya kazi zenu. Tayari mkoani hapa kuna viwanda vidogo na vya kati vingi kabla ya uwepo wa SIDO, hivyo kwa sasa naamini mtafanya vizuri zaidi,” alisema Mwijage.
Katika ziara hiyo, Mwijage alikabidhi kwa mkandarasi SUMA JKT eneo la ekari 25, ambako kutajengwa ofisi za kisasa zenye vyumba vya kufundishia na vyumba maalumu vya kuchakata bidhaa za chakula, alisema hiyo itasaidia bidhaa nyingi kupata vibali vya ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na dawa (TFDA).