32.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 21, 2024

Contact us: [email protected]

ShuleSoft, Selcom wazindua mfumo mpya wa malipo ya ada kwa urahisi na uhakika

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

KAMPUNI ya Shule Soft, ambayo inajihusisha na kuboresha mifumo ya uendeshaji wa shule nchini kwa kushirikiana na kampuni ya huduma za malipo ya Selcom zimezindua mfumo mpya wa malipo ya ada ambao unawawezesha wazazi au walezi kulipa ada kwa kutumia namba maalum inayotambua mwanafunzi aliyelipiwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo leo Jumanne Oktoba 8, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Shule Soft, Ephraim Swilla, amesema mfumo huo umetengenezwa ili kutatua changamoto ya kutopatikana kwa risiti au taarifa sahihi za wanafunzi waliolipiwa ada, ambayo imekuwa ikisababisha baadhi ya wanafunzi kurudishwa nyumbani au kushindwa kufanya mitihani.

“Mfumo huu ni maalum kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya fedha kutoonekana kwenye mifumo na matokeo yake wazazi kuendelea kudaiwa,” amesema Swilla na kuongeza:”Tumekuja na suluhisho hili, ambalo litasaidia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji ada na kuondoa malalamiko kwani itamtambua ni mwanafunzi yupi amelipa,”.

Swilla amefafanua kuwa mfumo huu unatoa urahisi kwa wazazi au walezi kulipa ada kupitia benki au mtandao wowote wa simu, huku fedha ikielekezwa moja kwa moja kwenye mfumo wa shule husika. Ameongeza kuwa mfumo huu hauhitaji makato yoyote, na utazinufaisha shule zaidi ya 450 za msingi, sekondari, na vyuo vya kati katika mikoa mbalimbali nchini.

Mkuu wa Masoko wa Selcom, Shumbana Walwa, akizungumzia faida za mfumo huo mpya, ameeleza kuwa unatatua changamoto ya fedha kutoonekana kwenye mifumo, ambayo imekuwa kero kubwa kwa wazazi na shule. “Uzinduzi wa hatua hii ni rahisi na utasaidia kufahamu malipo yaliyofanyika kwa uhakika,” amesema Walwa.

Mkuu wa Masoko wa Selcom, Shumbana Walwa, akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Aidha, alehamasisha shule na wazazi kutumia mfumo huo ili kuepuka usumbufu kwa wanafunzi wanaorudishwa nyumbani kwa sababu ya mifumo isiyosomana.

“Mfumo huu unapatikana katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mbeya, Arusha, Tabora, Dar es Salaam na Geita,” amesema Shumbana.

Kwa upande wake, Mkuu wa Biashara wa Shule Soft, Elisha Tengeni, amesema ulipaji wa ada kwa njia za kidigitali unasaidia kufuatilia na kubaini walipaji kwa wakati sahihi. Tengeni alitoa wito kwa shule kujiunga na mfumo huo ili kuondoa malalamiko na upotevu wa fedha ambao umekuwa ukiathiri baadhi ya shule.

Kupitia mfumo huo mpya, Shule Soft imejipanga kuboresha uzoefu wa wazazi na wanafunzi, na kuchangia katika kuongeza uwazi na ufanisi kwenye malipo ya ada kwa shule nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles