SERIKALI imepiga marufuku wamiliki wa shule binafsi kupandisha ada kuanzia Januari mwakani.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Serikali kutoa tamko la kufuta ada na michango mbalimbali kwa shule zake za msingi na sekondari.
Taarifa ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, profesa Sifuni Mchome, imepiga marufuku shule hizo kuongeza ada kwa mwaka wa masomo unaoanzia Januari 2016 hadi hapo watakapopata maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Elimu.
“Wale ambao tayari wameongeza ada kwa mwaka wa masomo wa 2016 bila kibali cha Kamishna wa Elimu, wizara haitambui ongezeko hilo kwa kuwa ni batili na hivyo zimefutwa,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema, waraka wa Elimu Na. 4 wa Mwaka 2008 uliweka viwango vya ada vinavyotozwa katika shule za msingi na sekondari za Serikali na zile zisizo za Serikali.
“Ada iliyowekwa kwa shule za binafsi za kutwa ni Shilingi 150,000 huku za bweni ikiwa ni Shilingi 380,000 kwa mwaka. Aidha waraka huo ulielekeza kwamba ongezeko lolote la ada lazima lipate kibali cha Kamishna wa Elimu kabla ya kuanza kutumika,” alisema.
Hata hivyo imegundulika kuna baadhi ya shule zisizo za serikali zimekuwa zikiongeza ada kila mwaka pasipo kupata kibali cha Kamishna wa Elimu.
Katika taarifa hiyo, Profesa Mchome alisema utamaduni huo wa kuongeza ada kila ifikapo mwishoni mwa mwaka umekuwa ukisababisha usumbufu mkubwa kwa wazazi/walezi na hata baadhi yao kushindwa kuendelea kusomesha vijana wao katika baadhi ya shule.
Taarifa hiyo ilisema kuwa, ada zote kwa shule zisizo za serikali zitabaki kama zilivyoidhinishwa na Kamishna wa Elimu.
Wamiliki wa shule hizo wametakiwa kuwasilisha taarifa kwa Msajili wa Shule aliyeko Idara ya Ithibati ya Shule inayoeleza kiasi cha ada kinachotozwa kwa sasa na tarehe shule ilipopata kibali kutoka kwa Kamishna wa Elimu kutoza kiwango hicho cha ada.
Novemba 27, Serikali ilitoa waraka wa elimu namba 5 wa mwaka 2015, ambao ulifuta ada zote zilizokuwa zikilipwa kwa ajili ya elimu ya sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha nne.