Na CLARA MATIMO, MWANZA
SHULE za msingi 15 za Serikali zilizopo Halmashauri ya Jiji la Mwanza, zimepatiwa msaada wa vifaa mbalimbali vya sekta ya elimu vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 50 kutoka shirika la Brac Maendeleao Tanzania, tawi la Mwanza.
Shirika hilo, limetoa msaada huo ikiwa ni utekelezaji wa mradi  wa kuwasaidia watoto wa kike  wanaokumbwa na changamoto, wakati wa masomo ‘Girls Education Challenge (GEC) ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2014 katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Singida, Tabora na Dar es Salaam.
Shule zilizopatiwa msaada huo, ni Iseni, Amani, Nyabulogoya, Pamba B na C, Mabatini A na C, Bugarika, Miembeni, Nyakabungo, Lake, Nyashana, Nyakurunduma, Tambuka Reli na Mbungani.
Akizungumza   wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo mwishoni mwa wiki iliyopita kwa Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula, Meneja  Mradi wa GEC, Kanda ya Ziwa, Shahinoor Rahman, alisema lengo la mradi huo ni kuwasaidia watoto wa kike waliokata tamaa ya kuendelea na masomo kutokana na changamoto mbalimbali.