YOHANA PAUL– MWANZA
WAZAZI na walezi wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari,wametahadharishwa kuwa makini na watoto wao hasa kike kipindi hiki cha likizo ya dharura ya janga la ugonjwa corona, kwani inaweza kuchangia ongezeko la mimba za utotoni.
Tahadhari hiyo, ilitolewa wiki iliyopita na Mkurugenzi wa Shirika la Kuteea Haki za Wanawake na Watoto la Kivulini, Yassin Ally wakati akizungumuza na waandishi wa habari juu ya hali na mwenendo wa vita ya mimba za utotoni.
Alisema uchunguzi uliofanywa na shirika hilo,umeibaini mimba nyingi za utotoni huwatokea katika kipindi kama hichi ambacho watoto wa kike wawapo nyumbani.
Alisema uzoefu unaonyesha, wakati wa msimu wa kusubiri matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la saba na kidato cha nne kwa wahitimu wa shule za msingi na sekondari, ndiyo tatizo hili hutokea zaidi.
“Natumia fursa hii kuwakumbusha wazazi na walezi wote misimu ambao huwa tunapokea kesi nyingi za mimba wa watoto wa kike, ni nyakati mbili, kwanza ni wakati wanafunzi wa darasa la saba wakiwa wanasubiri kujiunga kidato cha kwanza, na pili ni wakati kidato cha nne wanasubiri kujiunga na kidato cha tano au kwenda vyuoni.
“Kwa kuwa nyakati hizo zinafahamika, tayari tumeshafanya juhudi za kutosha kupunguza athari za mimba ya utotoni kwa vipindi hivyo viwili, lakini sasa likizo hii ya kupisha janga la corona imekuja ghafla na haijulikani itakuwa ni ya muda gani kwa hiyo tahadhari isipochukuliwa watoto wetu wa kike wataambulia mimba na kushindwa kurejea shule.
“Nawaomba wazazi pamoja na majukumu ya kila siku tuliyonayo, tuwajibike kuweka mazingira ya ulinzi yatakayozuia mtoto kuwa na uhuru wa kuzurura na kurandaranda pasipo kazi maalumu, tukifanya hivyo tutaweza kuwaepusha watoto wetu siyo tu na janga la corona lakini pia na janga la mimba za utotoni,” alisema Yassin.
Alisema walimu nao kwa nafasi yao, wanayo nafasi ya kuwasaidia wanafunzi kutumia muda mwingi majumbani kwao kwa kuwatumia maswari ya kufanya kwani kila kitu kinawezekana katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia, kwa kufanya hivyo itawezekana kuzuia watoto kukwapua mimba.