Na Seif Takaza, Kiomboi
Shirika lisilo la Kiserikali la Kikiristo la Compassion International Tanzania na Ushirika wenza wa Makanisa sita Klasta ya Iramba mkoani Singida limepongezwa kwa kuwahudumia watoto na vijana wanaoishi katika mazingira magumu.
Pongezi hizo zimetolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleimani Mwenda katika kikao cha wadau cha utambulisho wa huduma ya Maendeleo ya Mtoto na Kijana kilichofanyika mjini Kiomboi, Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ambapo wadau mbalimbali walihudhuria wakiwepo baadhi ya madiwani na baadhi ya wakuu wa idara na wachungaji wa makanisa sita waliopo kwenye Mpango.
Mwenda amesema Shirika hilo limekuwa na ufariji mkubwa kusaidia Watoto na vijana ambao wazazi na walezi wao wana hali mbaya kiuchumi.
“Mimi shuhuda kuhusu shirika hili la Compassion ambalo linasaidia sana Watoto na vijana wanaoishi katika mazingira magumu kwa kweli linanipa Faraja kubwa katika Wilaya yangu, hivyo sisi ni wajibu wetu kiwaunga mkono kwa hali na mali” amesema Mwenda.
Kwa Upande wake Mwezeshaji wa Shirika hilo wa Klasta za Iramba na Mkalama, Raphael Lyela amesema shirika la Compassion limeanza Novemba 2014 ambapo lengo lake ni kuwahudumia watoto na vijana waishio katika mazingira magumu.
Lyela alitaja vituo vilivyopo katika Klasta ya Iramba ni TAG Kiomboi, EATG Kiomboi, FPCT Shelui, KKKT Shelui, TAG Kinampanda na TAG Ulemo ambapo kila kanisa lilipatiwa watoto 200.
“Tumekuwa tukiwafundisha watoto na vijana masomo mbalimbali kama vile masomo ya uchumi ili kuhakikisha wanakuwa na stadi za maisha, waweze kumudu mazingira yao na kujitegemea.
“Pia masomo ya kijamii kuhakikisha vijana wanakuwa na tabia njema katika jamii na kimwili, vijana wanakuwa na afya njema na kiroho ambapo vijana wanakua na hofu ya Mungu na maadili mema katika jamii,” amesema Lyela.
Lyela amesema huduma hizo zimegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni huduma ya kunusuru maisha ya mama na mtoto na huduma ya ufadhili kwa watoto kuanzia miaka mitatu na kuendelea.
Naye, Yohana Kamwela ambaye ni Mwenyekiti wa Klasta ya Iramba akitoa taarifa yake alisema kuwa katika progamu zote mbili ina jumla ya washiriki 1,569 katika vituo kama ifuatavyo TAG Kinampanda 258, TAG Ulemo 261,TAG Kiomboi 243, EATGKiomboi 231, FPCT Shelui 241 na KKKT Shelui 245.
Kamwela alielezea muundo wa programu ambapo progaramu ya kunusuru maisha inahusu akina mama wajawazito hadi kufikia umri wa mtoto wa mwaka mmoja.
“Katika programu hii inatia mkazo katika maeneo ya afya wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua katika unyonyeshaji, uzazi wa mpango, elimu kwa wazazi na mshikamano wa mama na mtoto mchanga,” alisema.
Askofu Lameck pia alimshuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kumrudisha tena mchapa kazi wao, Suleiman Mwenda aliyehamishiwa Wilaya ya Monduli.
“Tunamshukuru Rais Samia kuturudishia mchapa kazi wetu tunakuombea kwa Mungu akusaidie ili tupate maendeleo na kudumisha amani nchini,” amesema Askofu Lameck.