25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Sheria ya mafao ya wastaafu isiligawe Taifa

TANGU ilipoanza kutumika Sheria Mpya ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Agosti Mosi, mwaka huu kumekuwapo malalamiko kutoka pande mbalimbali za nchi zikishutumu sheria hiyo ni mbaya ina lengo la kuminya fedha za wastaafu.

Akizungumza na Waandishi wa habari juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka  ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) Dk. Irene Isaka alifafanua kuwa tangu kuanza kwa Sheria hiyo Mpya ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, tayari wastaafu 4,900 wameshalipwa pensheni zaidi ya Sh. bilioni 379.

Dk. Iene alitanabaisha kwamba wastaafu hao wamelipwa pensheni hizo baada ya kukokotolewa fedha zao kulingana na sheria mpya inayowataka kuwalipa wastaafu hao asilimia 25 kwa mkupuo huku asilimia 75 iliyobaki ikilipwa kama mshahara wa kila mwezi kwa muda wote wa uhai wa mstaafu.

Mkurugenzi huyo aliendelea kufafanua kuwa pensheni hiyo haitolipwa kwa miaka 125 tu bali italipwa kwa muda wote wa uhai wa wastaafu na hata baada ya hapo wategemezi wataendelea kulipwa kwa kipindi cha miezi 36 yaani miaka mitatu.

Ni kweli kuanza kwa sheria hii mpya kumestua wafanyakazi wengi tulio kwenye vibarua na hata wanaotarajia kustaafu karibuni  ambao kwa mujibu wa sheria ya awali wastaafu walikuwa wakipata mafao yao kwa mkupuo na wengi walitumia mafao hayo pengine kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo kilimo kwa lengo la kuendeleza maisha yao ya kustaafu.

Sheria hii mpya ukiiangalia kwa haraka haraka ni kweli utaiona inaumiza na pengine unaweza ukaiona haina lengo la kumsaidia mstaafu zaidi ya kuwa na lengo la kuzidi kumfanya aendelee kuwa tegemezi ilhali akiwa na akiba yake ambayo endapo angepatiwa kwa mkupuo angeweza kujipangia aitumie vipi. Hawa tusiwabeze wanayo haki ya msingi ya kuwaza hivyo kwani hiyo ni akiba yao na jasho lao walilolitumikia nyakati za ujana wao.

Lakini tukija kwenye uhalisia. Tumeshuhudia wastaafu wengi sana wa nchi hii wanaishi maisha yenye furaha baada ya kustaafu kwa miaka michache tu baada ya kustaafu. Furaha hiyo hutokana na zile fedha za mkupuo wanazozipata ambazo wengi wao huanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kushirikiana na ama watoto ndugu wa karibu na marafiki.

Miradi hiyo haichukui muda kuendelea kutokana na kudhulumiwa na washirika  wao na  hii hutokana na wengi wao kutokuwa na elimu ya ufanisi na ya kutosha ya namna ya kuiendesha hiyo miradi waliyoibuni na matokeo yake miradi hiyo inakufa polepole.

Hali hiyo haiishi hapo kwa kufa kwa miradi ya uwekezaji waliyoibuni, hatari inakwenda zaidi wengine hufikia kurudi nyuma kiuchumi na matokeo yake baadhi yaao wanarudi kuwa ombaomba kwa wategemezi wao na wengine hufariki dunia wakiwa maskini.

Kama alivyosema Mkurugenzi wa SSRA, Dk. Irene, malalamiko yaliyopo sasa na yaliyopokelewa yanaonesha yanatokana na na wanachama wa PSPF waliokopa mikopo ya nyumba kwa kutegemea kwamba watalipwa mkupuo wa asilimia 50.

Kwa kupokea asilimia 25 wameona hautoshi kulipa deni la nyumba na kubakiwa na kiasi cha fedha kitakakachotosheleza mahitaji mengine.

Hawa wanayo haki kulalamikia hili, lakini kwa mujibu wa Dk. Irene jambo hilo wanalifanyia kazi kuona kamba mifuko inabuni namna bora zaidi zenye unafuu katika ulipaji wa deni hilo la nyumba na kuleta unafuu kwa wanachama.

Wakati haya yakiendelea kwa wastaafu, tunawasihi viongozi wa kisiasa kuacha kabisa kuligawa Taifa kwa kutumia kigezo cha wastaafu ambao ndio jeshi kubwa la Taifa. Huu ni wakati wa kuliunganisha Taifa kwa kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kuona kuwa sheria mpya ya mafao ya wastaafu haiwachanganyi walengwa.

Wapo wanasiasa wanaopenda kutafuta ‘kiki’ pale inapotokea Serikali imekuja na hoja ya msingi wakiwa na lengo la kuvuruga vichwa ili iwe mtaji wa kujipaisha kisiasia, hii sio sawa.

Ninaamini sheria hii mpya ya mafao ka wastaafu haina lengo la kumminya mstaafu ambaye amelitumikia Taifa lake kwa uadilifu, tusipoteze maana halisi na kuingiza siasa kwenye kila jambo la msingi.

Ni muhimu sana kwa Watanzania kuepuka kufuata mkumbo, ni vyema kutumia vichwa vyetu kufikiri kwa kiwango kikubwa kila kinachokuja mbele yetu, pale ambapo tunadhani tunao wajibu wa kuishauri Serikali tutumie wajibu wetu huo badala ya kukurupuka.

Naamini Serikali yetu sikivu yale yote ambayo yameonekana kuleta utata kwa wastaafu watatumia busara na weledi kuyatafutia ufumbuzi.

Lakini pia nguvu kubwa ielekezwe katika kutoa elimu ya sheria hii mpya ili kuacha pengo hili kuzibwa na wanasiasa wanaotaka kuupotosha umma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles