Na Mwandishi Wetu
IMEKUWA kawaida siku zote kwa Serikali kutaka ardhi kutoka kwa wanakikiji kwa matumizi ya maendeleo, ikiwa tayari kulipia fidia na wananchi kuhama, lakini kwa mara ya kwanza kabisa mamlaka ya serikali imegomewa na kuleta sintofahamu kwa wadau wa hatima ya mvutano huo wa nmana yake.
Wanakijiji Bagamoyo wamegoma kuhama kwa namna yoyote kwenye hifadhi ya Taifa ya Saadani wakidai hawana haja kwani ardhi ni yao na hawako tayari kuhama hata kama Serikali iko tayari kulipa fidia ili kupisha upanuzi wa Mbuga ya Taifa ya Saadani kwa manufaa makubwa ya uchumi wa watu wa Bagamoyo na Taifa kwa ujumla.
Wananchi wa kitongoji cha Uvinje kilichomo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Bagamoyo mkoani Pwani, wamegoma kuhama na hawako tayari kuhama wala kulipwa fidia ili kupisha hifadhi hiyo amabayo imeanza kupata umaarafu kwa utalii wa ndani kwa watu wa Dar es Salaam hasa mwishoni mwa wiki.
Kitongoji cha Uvinje kilianza sokomoko hilo na Serikali kuanzia mwaka 2005, ambapo iliamuliwa kuwa vijiji vinane hivyo viondolewe kwenye eneo la hifadhi ili kufanya mambo yawe murua baada ya hifadhi hiyo kupandishwa daraja kutoka pori la akiba na kuwa hifadhi kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 281 la Septemba 16, 2005.
Kaimu Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Hassan Akida, alisema mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japheth Hasunga, aliyetembelea hifadhi hiyo kuwa wakazi wa eneo hilo hawako tayari kuhama na wala kulipwa fidia kwa vile ni ardhi yao toka enzi za mababu zao.
“Tumesema hapa ndiyo kwetu mnataka kutuhamisha mtupeleke wapi wakati sisi tumezoea maisha yetu hapa,” alihoji Akida.
Aliongeza kuwa kitongoji hicho kimekuwapo kwa muda mrefu na waliishi bila shida hadi pale pori hilo lilipobadilishwa na kuwa hifadhi ya Taifa.
“Wakati hili ni pori la akiba tuliishi vizuri tu na wazazi wetu walikuwa wafanyakazi wa pori. Lakini tangu iwe hifadhi imekuwa taabu. Sasa tunafukuzwa wakati tumezaliwa hapa na wazazi wetu wamezikwa hapa hapa,” alisisitiza Akida.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Saadani, Adam Mwandosi, alisema mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu na umekuwa ukileta chuki kati ya Serikali na wananchi.
Alisema wananchi wa eneo hilo muda mwingine wamekuwa wakimwona hata yeye mwenyekiti wao kama anawasaliti kwa vile tangu mgogoro huo ulipoanza, viongozi wengi wamekuwa wakifika lakini wamekuwa hawana majibu ya kumaliza mgogoro huo.
Hata hivyo, Mhifadhi Mkuu wa Saadani, Stepahano Msumi, amesisitiza kuwa kitongoji hicho kimo ndani ya hifadhi kinyume cha sheria. Alisisitiza kuwa Sheria ya Hifadhi za Taifa hairuhusu makazi ya watu ndani yake.
Wadadisi wa masuala ya uhifadhi wanyama wanadai Mhifadhi amesahau kuwa kwenye Mbuga ya Serengeti Wamasai wanaishi na wanyama ndani ya Mbuga ya Serengeti na dhana hiyo kuonekana kivutio kwa watalii, lakini kwa gharama ya mbuga kwani hawaruhusiwi kulima chakula na kufanya maendeleo mengine yoyote ya maisha na hivyo kutegemea Mamlaka ya Hifadhi Wanyama kwa kila kitu.
“Kwa ufupi tu ukiangalia Tangazo la Serikali linaonyesha kuwa eneo lote la Kitongoji cha Uvinje liko ndani ya hifadhi. Ni kweli lilikuwa eneo la watu ambao walikuwa watumishi wa Pori la Akiba tangu lilipoanzishwa mwaka 1968. Waliombwa kuondoka lakini waliendelea kuongezeka,” alisema.
Historia
Alisema Mhifadhi kuwa katika makubaliano, iliamuliwa kuwa walipwe fidia kwa taratibu lakini hata hivyo licha ya kutekeleza utaratibu wa fidia bado wamegoma kuipokea.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bagamoyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hasunga, aliwaambia wananchi hao kuwa lengo la ziara yake ni kutaka kuwasikiliza juu ya mgogoro huo na si kuwahamisha.
“Mimi ni mgeni kidogo kwenye wizara hii, nimekuja kuangalia si kuwahamisha kwa kuwa sijui eneo hili lina ukubwa kiasi gani na lina kaya ngapi, lakini nimekuja kutembelea hifadhi na maeneo yote yenye changamoto,” alisema.
Alisema amekwenda kuwasikiliza ili aweze kujua jinsi mgogoro ulivyo kwa sababu hakutaka kusikia upande mmoja wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Saadani ni hifadhi pekee ya Taifa nchini, Afrika Mashariki na Afrika yenye na mipaka na fukwe za bahari, kwani inatazamana na Bahari ya Hindi na fukwe zake zinakutana na uoto wa asili wa nchi kavu wakati kusini kwake unapita Mto Ruvu na katikati ya mbuga unapita mto Pangani kwa upande wa Kaskazini.
Hifadhi hiyo inapatikana katika mikoa ya Tanga na Pwani na uwepo wake ni matokeo ya pori la akiba la Saadani, ranchi ya Mkwaja na sehemu ya kaskazini, sambamba na akiba ya msitu wa asili wa Zaraninge.
Kama alivyosema mwenyewe Naibu Waziri Hasunga, alikuwa anatafiti ukweli wa mambo na ameupata na hivyo atajaribu kutumia Sheria kutekeleza mfumo wa kumaliza tatizo hilo lenye hisia kali kwa wakazi wake na kufanya maamuzi bila kuogopa upinzani aliouona, kwani Serikali ni moja na si vizuri kuwa na kupindapinda sheria.