NA OSCAR ASSENGA, TANGA
ULIPUAJI wa milio kwenye pikipiki (Exose) maarufu kama jango moshi, umetajwa kuwa miongoni mwa ugaidi mpya unaoitesa jamii ya Watanzania wengi ambao wameshindwa kuishi kwa amani.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limetakiwa kuona namna ya kudhibiti hali hiyo.
Hayo yamesemwa jana na Sheikh wa Msikiti wa Bilal Muslim wa mjini Tanga, Mohamed Mbaraka, wakati wa kikao cha pamoja baina ya viongozi wa dini na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba.
Alisema jambo hilo halina tofauti na ugaidi kutokana na kuwa milio hiyo imekuwa ikilipuliwa hadi saa nane usiku watu wakiwa wamelala majumbani mwao.
“Ukiangalia ndugu yetu Kamanda wa Polisi, watu wamekuwa wakifikiria ugaidi ni vitendo vibaya, viovu tu, hata suala la ulipuaji wa milipuko kwenye pikipiki maarufu kama jango moshi, nao ni hatari,” alisema.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Moravian Chumbageni, Ibrahim Nzowa, aliunga mkono hoja hiyo na kusema jambo hilo ni hatari.
Naye Kamanda Wakulyamba aliwataka viongozi wa dini kuacha kuwakumbatia watu wachache wanaotumia mianya ya dini kufanya vitendo viovu.
“Viongozi wa dini wana nguvu za Mwenyezi Mungu na kiroho ambazo wanaweza kuzitumia kwa ajili ya kuibadilisha jamii… umoja wenu huu ni muhimu katika masuala ya usalama,” alisema.