27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WAZEE EAC WAIBUKIA MAHAKAMA YA AFRIKA

Na ASHA BANI – Dar es Salaam

WASTAAFU wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wamefungua kesi ya madai katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, msemaji wa wastaafu hao, Ahmed Kabunga, alisema madhumuni ya kufungua kesi dhidi ya Serikali ya Tanzania, ni kutoridhika kwao juu ya hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Rufaa.

Alisema hukumu hiyo namba 73/2014 inaeleza kuwa Serikali ya Tanzania ilikwishawalipa madai yao yote.

“Kwa nguvu zote, tunapinga uamuzi huo ambao haukuzingatia haki zetu za msingi na za kibinadamu, tumefanya hivyo baada ya kumaliza ngazi zote za utoaji wa haki katika mahakama zetu, hatujapata haki yetu,” alisema Kabunga.

Alisema kwa sababu Serikali kama msimamizi wa mali za iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, sio tu imeshindwa bali imekataa kutumia sheria, masharti na kanuni za jumuiya hiyo kukokotoa na kulipa stahiki za wazee hao, kwa kuwa sheria hizo na kanuni za ajira ndizo zilizotawala.

Kabunga alisema ikumbukwe baada ya jumuiya hiyo kuvunjika mwaka 1977, aliteuliwa msuluhishi, Dk. Victor Umbritch, ili kugawa mali na madeni yake.

“Aliweka utaratibu tena wa wazi wa kulipa madeni, miongoni mwao yakiwamo malipo yetu ya wafanyakazi wa zamani tuliyotakiwa kulipwa kwa thamani halisi,” alisema Kabunga.

Alisema baada ya kuvunjika jumuiya hiyo, wengi wa wafanyakazi ambao walikuwa bado vijana wakati huo, waliajiriwa upya katika idara mbalimbali za Serikali na mashirika ya umma yaliyoundwa ili kuziba pengo na kuendelea na huduma zilizokuwa zikitolewa na EAC, kwa ahadi kwamba watalipwa haki zao baada ya kustaafu.

Kabunga alisema walipoanza kustaafu kuanzia miaka ya 1990, waliambiwa na Serikali hakuna malipo na hawastahili kulipwa.

Alisema kutokana na kauli hizo, wastaafu hao waliunda umoja na kufungua kesi mwaka 2003 ili kudai haki zao.

“Serikali ilipobaini ina kesi ya kujibu,iliomba wamalize suala hilo nje ya mahakama.

“Kwa nia njema, wastaafu kwa kuamini Serikali yetu tulikubali wazo hili, lengo letu ni kulipwa stahiki ya haki zetu na sio kulumbana na Serikali na mahakama nayo ikaridhia hilo.

“Kitendo cha kukubali kuzungumza nje ya mahakama kupitia kamati zilizoundwa kati ya Serikali na wawakilishi wa wastaafu, kuliipa mwanya Serikali na kutengeneza mkataba wa makubaliano na kuweka pembeni makubaliano ya awali  yaliyoitwa mwafaka,” alisema Kabunga.

Alisema hadi sasa, ni miaka 40 tangu EAC ivunjike na zaidi ya nusu ya wazee wamefariki dunia na kuacha watoto na wajukuu zao wakihangaika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles