MWEZI Februari umeanza vibaya kwa mastaa kadhaa kwenye kiwanda cha burudani ndani ya Bongo. Najua mnafahamu wazi kile kilichotokea wiki iliyopita na kupelekea baadhi ya wasanii wa muziki na filamu kutupwa rumande, tuyaache hayo.
Kilichofanya nitumie wino wangu kuyaandika haya unayoyasoma ni jinsi ukubwa wa tatizo la ukosefu wa ushirikiano linavyoitafuna tasnia ya burudani. Ukitaka ujue una idadi gani ya marafiki wa kweli na una kiwango kikubwa kiasi gani cha marafiki wanafiki basi mwombe sana Mungu akupe tatizo.
Naam, nadhani hili ni somo pana kidogo ila kwa kiasi chake nitakufungua akili ili kile nilichonacho niweze kukiweka ndani yako. Kwa muda mrefu wasanii hasa wa filamu wamekuwa wakilalamika kuibiwa kazi zao. Moja ya upenyo unaotumika kuwaibia wasanii wameutengeneza wenyewe.
Ushirikiano ndiyo kitu pekee kilichokosekana. Kila msanii mkubwa wa filamu anafanya kazi kivyake na mbaya zaidi wakishapata senti mbili kutokana na mauzo machache ya filamu zao hukutana kwenye vilinge vya bata na kuponda raha. Hao hao waliopeana ushirikiano kwenye ulabu wanashindwa kupeana ushirikiano kwenye matatizo yao binafsi kama wanadamu.
Wema Sepetu ni miongoni mwa mastaa waliokubwa na kadhia ile, alitiwa nguvuni na kukaa rumande takribani juma zima mpaka ile juzi alipoachiwa kwa dhamana. Nadhani unawafahamu marafiki zake wale anaoponda nao raha, jiulize ni wa ngapi walimtembelea akiwa rumande hata siku ile anapandishwa kizimbani?
Jicho langu lilimuona Shamsa Ford, huyo ndiyo msanii wa kike maarufu aliyeonekana eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati Wema anapandishwa kizimbani kusomewa mashtaka yake na mwisho kufanikiwa kuchomoka kwa dhamana.
Nilitarajia kuwaona ‘Team Wema’ wote wakiwa pale lakini sikufanikiwa kuwaona na badala yake waliishia kumpa pole kwenye mitandao ya kijamii na wengine wakakausha kabisa kana kwamba hakuna kilichotokea. Hii ni roho ya ajabu mno.
Hongera Shamsa kwa kuonyesha utu, wewe ni mfano wa kuigwa na marafiki wengine wa Wema, najua sapoti uliyompa Wema ilimfariji mno hata kama yeye hatakushuru basi Mungu wake atakulipa.