28.6 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAWEKA PINGAMIZI KESI SHERIA YA HABARI

Na MASYENENE DAMIAN–MWANZA

SERIKALI kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), imepinga mahakamani shauri la kikatiba lililofunguliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na Kampuni ya Hali Halisi Publishers ya kupinga sheria ya huduma za vyombo vya habari namba 12 ya mwaka jana lisisikilizwe.

Shauri hilo namba mbili la mwaka huu lililofunguliwa Januari 18, mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, linasikilizwa na Jaji wa mahakama hiyo, Joaquine De –Mello, ambaye alisema anataka limalizwe ndani ya siku 30.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi nje ya mahakama hiyo, Wakili wa mlalamikaji, Jebra Kambole, alisema shauri hilo ambalo liko katika hatua za awali za kusikilizwa litatolewa uamuzi Machi 9, mwaka huu baada ya jaji kusikiliza majibu ya pande zote mbili.

“Mwanasheria Mkuu wa Serikali alileta majibu yake na kuyawasilisha mahakamani Februari 8, mwaka huu na kutuwekea mapingamizi matano na tumekubaliana na mahakama kwa pamoja yasikilizwe kwa njia ya maandishi ambapo Serikali italeta hoja zake Februari 16, mwaka huu na sisi majibu yetu tutayapeleka Februari 23, mwaka huu na kama Serikali itakuwa na nyongeza itaziwasilisha Machi 2, mwaka huu,” alisema.

Mapingamizi yaliyowasilishwa na Serikali ni pamoja na kwamba mahakama haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo, walalamikaji hawana uwezo wa kisheria wa kufungua shauri hilo, sheria ya kuendeshea shauri hilo imenukuliwa vibaya (bila kutaja ni sheria gani), viapo vya walalamikaji vina kasoro na walalamikaji hawana hoja za msingi za kuifanya mahakama kusikiliza shauri hilo hivyo kuiomba mahakama ilifute shauri hilo kwa gharama.

Katika shauri hilo, AG aliwakilishwa na Mawakili Mark Mulwambo akisaidiwa na Castus Ndamugoba, huku upande wa walalamikaji ukiwakilishwa na mawakili Kambole na Edwin Hans.

Katika shauri hilo la kikatiba walalamikaji wanadai ufafanuzi wa Mahakama juu ya sheria mpya ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kukiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 18 ambapo jumla ya vipengele 26 vya sheria hiyo vinapingwa.

Vifungu vinavyolalamikiwa katika sheria mpya ya huduma za vyombo vya habari namba 12 ya mwaka 2016 ni pamoja na 7(2) (b) (iii) (iv) na (v), 7 (3) (a),(b),(c), (f), (g),(h),(i),(j), 8, 13, 14, 19, 20, 21, 24, 25, 26, 35, 36, 37, 38, 39, 40, 50, 52, 53, 54, 58 na 59, ambapo mlalamikaji mkuu katika kesi hiyo ni UTPC akishirikiana na Hali Halisi Publishers ambao wanatetewa na jopo la wanasheria sita wakiongozwa na Jenerali Ulimwengu, Fulgence Massawe, Edwin Hans, Kambole, Fransic Stolla na Mpale Mpoki.

 

Naye, Ulimwengu ambaye ni mmoja wa wanasheria wa kesi hiyo, alisema sheria hiyo inanyonga uhuru wa kupashana habari hivyo wanapinga unyongaji huo wa haki ya kutoa na kupata habari.

“Hatutashadadia unyongaji huu na hatuwezi kushiriki kutunga kanuni zake kwa maana tutakuwa tumeshiriki unyongaji wa uhuru wa kupashana habari,” alisema.

Kwa upande wake, Kambole, alisema kesi hiyo ni tofauti na ile iliyofunguliwa na Tume ya Haki za Binadamu katika Mahakama ya Afrika Mashariki kwa kuwa ile inahoji uhalali wa uvunjaji wa mkataba wa Afrika Mashariki.

“Ile haijafunguliwa Dar es Salaam wala mahakama za hapa nchini, hii ya kwetu ni ya kikatiba ya sheria ya huduma za vyombo vya habari dhidi ya Katiba ya nchi kukiuka haki ya wananchi kupata habari na uhuru wa kujieleza, hivyo tunataka mahakama itafsiri kama ni kweli Katiba imekiukwa ama la,” alisema.

Naye Makamu wa Rais wa UTPC, Jane Mihanji, alisema hatua hiyo ni kutetea masilahi ya umma katika kupata habari kwa kupata ufafanuzi wa kisheria kutoka mahakamani juu ya kukiukwa kwa katiba na kusisitiza kwamba waliipinga sheria hiyo tangu awali na waliomba kuongezewa muda wa kuijadili lakini hawakusikilizwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles