KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kukutwa na dawa za kulevya inayomkabili Shamim Mwasha na mumewe, Abdul Nsembo, wameendelea kuita mashahidi ambapo shahidi wa sita ameeleza jinsi alivyopeleka sampuli za unga kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya uchunguzi.
Shahidi huyo ambaye ni Ofisa kutoka Mamlaka ya Udhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Juma Suleiman, alidai hayo jana katika Mahakama Kuu kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, mbele ya Jaji Elinaza Luvanda.
Akiongizwa na Wakili wa Serikali, Costantine Kakula, Suleiman alidai Mei 2 mwaka 2019, alikabidhiwa vielelezo na Ispekta Johari pamoja na fomu ya uwasilishaji wa sampuli katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Shahidi alidai alipopeleka sampuli hizo zilipokelewa na mkemia aliyemtaja kwa jina la Fidelis Segumbo kwa ajili ya uchunguzi.
“Sampuli ambazo ni vielelezo vilikuwa ni bahasha tano, katika uchunguzi wa awali mkemia alibaini kuwa baadhi ya vielelezo ni dawa za kulevya aina ya heroin, alivifunga kwa lakili ya mkemia, aligonga mhuri na kuweka sahihi yake,” alidai Suleiman.
Alidai, baada ya uchunguzi vielelezo hivyo vilivyokuwa ndani ya bahasaha na kupewa alama A, B, C, D, E, alivirudisha ofisi za DCEA na kumkabidhi Johari.
Katika kesi hiyo, washitakiwa ni Shamimu ambaye ni mmiliki wa Blog 8020 Fashion na mumewe mfanyabiashara Abdul Nsembo.
wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride zenye uzito wa gramu 232.70
Washtakiwa hao ambao ni wakazi wa Mbezi Beach, walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani Mei 13, mwaka jana.
Inadaiwa Mei Mosi, mwaka jana wakiwa eneo la Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa na dawa hizo.