KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeanza kusikiliza ushahidi wa kesi ya kushawishi rushwa ya Sh milioni 200 inayowakabili maofisa wa polisi wapelelezi, Inspekta Msaidizi wa Polisi, Shaban Shillah na wenzake watatu.
Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Inspekta Fatuma Mbwana, alitoa ushahidi jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashidi Chaungu kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Maghela Ndimbo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Ofisa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Kawe, Emmanuel Njegele na wapelelezi wengine; Inspekta Msaidizi, Shaban Shillah, Joyce Kitta na Ulimwengu Rashidi.
Inspekta Fatuma alidai yuko katika Kitengo cha Uchunguzi wa Maandishi na Mei 16 mwaka jana akiwa katika maabara ya uchunguzi alipokea barua iliyoambatana na vielelezo vya kufanyiwa uchunguzi.
Alidai vielelezo hivyo ni maelezo yaliyotolewa Polisi na Diana Thomas Naivasha anayedaiwa kuombwa rushwa, saini ya Diana na saini ya mshtakiwa Joyce.
Inspekta Fatuma anadai alitumia macho na mashine kufanya uchunguzi huo Mei 27 mwaka jana na kubaini kwamba maelezo yaliyotolewa polisi yanayodaiwa kuandikwa na kusainiwa na Diana si ya Diana bali yaliandikwa na kusainiwa na mshtakiwa Joyce.
Pia uchunguzi ulibaini kwamba saini ya Diana na mshtakiwa Joyce zinatofautiana na kwamba matokeo hayo ni kutokana na tabia za maandishi.
Inadaiwa mshtakiwa Joyce alighushi maelezo na saini akionyesha kwamba yalitolewa na kusainiwa na Diana.
Katika maelekezo hayo inadaiwa iliandikwa kwamba ‘Mimi Diana Naivasha nimezaliwa Dar es Salaam mwaka 1972, naishi Msasani, wazazi wote wawili walifariki na katika uzima wao walikuwa wawindaji, walikuwa wanatoa huduma za dawa za mifugo na walikuwa na kampuni inaitwa Interpol Adventures Safari’.
Maelezo hayo yanasema kwamba wazazi wake walifariki na mwaka 2011 kampuni ilibakia mikononi mwa watoto, hawakuendelea na shughuli hizo ambapo nyumba ya wazazi wao iliyopo Afrika Sana aliipangisha.
Inspekta Fatuma alidai kuwa maandishi ya maelezo hayo yote na saini ni ya mshtakiwa Joyce na si Diana.
Akihojiwa na Wakili Peter Kibatala, alidai kwamba barua na vielelezo kwa ajili ya Uchunguzi alivipokea kutoka kwa Mchunguzi wa Takukuru, Colman Lubis.
Shahidi alidai alichoandika ni maoni yake na kwamba barua iliyomtaka kufanyia uchunguzi vielelezo hivyo aliiacha ofisini.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 15.
Katika hati ya mashtaka inadaiwa Desemba 17, 2018 maeneo ya Rainbow Social Club, Kinondoni, wakiwa maofisa wa uchunguzi, waliomba rushwa ya Sh milioni 200 kutoka kwa Diana kama kishawishi cha kutokuchukuliwa hatua za kisheria kwa kosa la kukutwa na nyara za Serikali.