30 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Takukuru yazimulika kampuni zilizolipwa fedha hewa

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Dodoma imebaini Kampuni ya Leostart Engineering Co Ltd kulipwa zaidi ya Sh milioni 120 hewa katika mradi wa maji katika Kijiji cha Mlongia, Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.

Kutokana na hali hiyo, kampuni hiyo imetakiwa kulipa fedha hizo ambapo hadi sasa imelipa jumla ya Sh milioni tano.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Mkuu wa Takukuru mkoani Dodoma, Sostenes Kibwengo alidai kuwa mradi wa maji katika Kijiji cha Mlongia wilayani Chemba  wenye thamani ya Sh milioni 579.3 ulianza mwaka 2013 na kukamilika mwaka 2014.

Hata hivyo alisema mradi huo haukuwa ukitoa maji hadi Takukuru ilipofuatilia na mkandarasi Leostart Engineering Co. Ltd kurudi katika eneo la mradi na kufanya marekebisho na sasa mradi unatoa maji.

“Ufuatiliaji wetu ulibaini pamoja na mradi kuwa chini ya kiwango, pia mkandarasi alilipwa Sh milioni 120.2 zaidi ya thamani ya kazi zilizofanyika, hivyo pamoja na kurekebisha mradi ili utoe maji, tayari ameanza kurejesha serikalini fedha alizozidishiwa ambapo mpaka sasa ameishalipa Sh milioni tano,” alisema Kamanda Kibwengo.

Alieleza kuwa wanaendelea kufuatilia utokaji wa maji na kuhakikisha mkandarasi huyo anarejesha kiasi cha fedha kilichosalia.

Pia, alisema Takukuru Mkoa wa Dodoma imeokoa kiasi cha Sh milioni 94.7 huku ikiendelea kuchunguza miradi minne yenye thamani ya Sh milioni 261.042 ambayo imebainika kuwa na viashiria vya rushwa na udanganyifu.

Kamanda Kibwengo alisema fedha  hizo ni kutoka katika miradi 26 ya maendeleo yenye thamani ya jumla ya Sh bilioni 6.6 katika sekta za elimu, maji, ujenzi, mifugo, kilimo na umwagiliaji, mapato na utawala.

“Tumefuatilia na kukagua miradi 26 ya maendeleo yenye thamani ya jumla ya Sh bilioni 6.6 katika sekta hizo ambapo tumefanikiwa kuokoa Sh milioni 94.7 baada ya kuwa zimechepushwa katika miradi hiyo na hivyo kuongeza thamani ya jumla ya Sh milioni 261.042, ina viashiria vya rushwa na udanganyifu.

“Ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo una faida kubwa kwani pamoja na kuokoa rasilimali zinazochepushwa, unasaidia miradi hiyo kukamilika kwa wakati na kwa viwango stahiki, lakini zaidi ufuatiliaji huo unachochea ushiriki wa wananchi katika kuisimamia,” alisema Kamanda Kibwengo.

Alisema kuwa katika kipindi hicho wameokoa jumla ya Sh milioni 297.1 pamoja na kushikilia magari matatu kutokana na ufuatiliaji wa kazi mbalimbali ili kuhakikisha fedha na mali za umma zinatumika kulingana na taratibu sahihi na siyo kufujwa.

“Sh milioni 143.5 ziliokolewa kutoka kwa viongozi na wanachama 67 wa vyama sita vya akiba na mikopo waliokuwa wanadaiwa kwa muda mrefu na magari matatu aina ya Toyota Hiace yalichukuliwa kutoka kwa viongozi wa Saccos moja waliokuwa wanatumia kwa faida binafsi,” alisema Kamanda Kibwengo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,968FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles