24.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Seti ya kwanza ya vichwa mchongoko vya Treni ya SGR vyatua nchini

*Profesa Mbarawa asema historia imeandikwa

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

TANZANIA imeandika historia nyingine baada ya kuwasili kwa seti ya kwanza ya vichwa vya mchongoko vya Treni ya umeme inayoitwa Electric Multiple Unit (EMU) kwa ajili ya kuanza kwa huduma ya usafiri wa reli ya mwendokasi nchini(SGR).

Akizungumza leo Aprili 3, 2014 jijini Dar es Salaam wakati wa mapokezi ya seti hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kichwa kimoja cha mchongoko kina uwezo wa kubeba behewa nane.

“Watanzania walikuwa wanazungumzia sana vichwa vya mchongoko sasa leo ndio mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu tunapokea kichwa cha mwanzo chenye shepu ya mchongoko, nafikiri katika Afrika Mashariki na kati hivyo ndio vichwa vya mwanzo vya aina hii,” amesema Profesa Mbarawa.

Amesema Serikali imeagiza jumla seti 10 ya vichwa hivyo vitakavyogharimu dola za kimarekani milioni 190 na kila seti moja itakuwa na uwezo wa kuchukua mabehewa manane ambayo kwa wakati mmoja yana uwezo wa kubeba abiria 589.

“Kwa kuwa reli yetu ya kisasa ya SGR mbali na yale mengine lakini itatumia zaidi mabehewa na vichwa hivi kwa kusafiri kutoka Dar es Salaam- Morogoro na Morogoro -Dodoma na vitakuwa vinatumika zaidi katika safari fupi na wakati tukiwa tunakwenda Mwanza tutatumia yale mengine ya umeme.

“Leo tumepokea seti ya kwanza na kila mwezi tutakuwa tunapokea seti hizo hadi zitakapokamilika kwa ujumla ni seti 10 ambazo zinatengenezwa Korea ya Kusini na kampuni ya Hyundai Rotem,” ameeleza.

Mbarawa amesema amefurahi kuwasili kwa seti hiyo kwa sababu Watanzania walikuwa wanasema sana hivyo ni vyema wakatambua kuwa serikali bado inaendelea kufanya makubwa kwa watu wake.

“Mimi nimefurahi kwa sababu Watanzania walikuwa na maneno mengi, wamesema maneno mengi, wametusema sana lakini ukweli ukidhihiri uongo unajitenga, serikali yetu inafanya mambo makubwa kila siku ilikuwa hamtuamini wengine wameandika mambo mengi kwenye mtandao lakini leo majibu yanaonekana,” amesema.

Amesema treni hiyo imetengenezwa kwa kutumia kasi ya 160 hivyo wanatarajia kufanya majaribo hatua kwa hatua.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Amina Lumuli amesema treni hiyo itafanyiwa majaribio ili kujiridhisha na utendaji wake kabla ya kuanza rasmi kutoa huduma kwa jamii.

Amesema hadi sasa wameshapokea mabehewa 65 vichwa tisa vya umeme kwa ajili ya kuanza kuwahudumia wananchi ambapo kutakuwa na EMU na vichwa vya kawaida vya umeme katika kutoa huduma.

“Tunahitaji kufanya majaribio kuona uwezo wa njia na mabehewa yenyewe tumejipanga kutoa huduma ya uhakika kwa wananchi,” amesema.

Naye Meneja Mradi wa Manunuzi wa Treni za Mwendokasi 10, Calvin Kimario amesema treni hizo ni za kipekee na zimezingatia usalama na miundombinu yake ni rafiki kwa watu wote ikiwemo wenye mahitaji maalum.

Treni hiyo inauwezo wa kumuongoza dereva katika maeneo ambayo yanahitaji kupunguza mwendo na huwa inapunguza yenyewe hata kama dereva akiwa bado kwenye ‘speed’ ya 160.

“Hizi treni ni za kipekee sana zinaweza kumuongoza dereva kupunguza mwendo kwenye maeneo ambayo yanahitaji kufanyika kwenye makaravati lakini pia treni hii inatumia umeme mwingi ambao ni salama na hauna madhara kwa watumiaji,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles