25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yazidi kuwakomalia wenye visima vya maji

Na Aziza Masoud, Dar es Salaam

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo, amewasisitiza wamiliki wa visima ambavyo vimezidi mita 15 kuhakikisha wanafuata sheria kwakukata vibali ambavyo vitawaelekeza kulipa ada ya matumizi ya maji kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Profesa Mkumbo, ametoa msisitizo huo siku chache baada ya Ofisa Maji wa Bonde la Wami/Ruvu, Simon Ngonyani,  kutangaza operesheni ya kuwatafuta na kuwachukulia hatua za kisheria wamiliki wa visima visivyolipiwa ada ya matumizi ya maji.

Msisitizo huo aliutoa jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambapo alifika kwa lengo la kutoa taarifa kuhusu hali ya upatikanaji wa maji katika jiji hilo.

Alisema mtu yeyote ambaye amechimba ama anatarajia kuchimba kisima  kinachozidi matumizi ya kawaida yaani zaidi ya mita 15, anapaswa afuate taratibu za kuchukua kibali.

“Kwa watu wanaochimba visima vya maji kwa ajili ya matumizi ya kawaida hahitaji kibali, lakini wale wanaotumia visima ambavyo vipo zaidi ya mita 15, lazima wafuate taratibu ikiwemo kulipia huduma hiyo,” alisema Profesa Mkumbo.

Alisema Serikali imeweka utaratibu huo muda mrefu isipokuwa umeanza kutiliwa mkazo kwa sasa kutokana na hali ya upatikanaji wa huduma za maji kuwa nzuri.

Alisema lengo si kuwakomoa wananchi bali ni kumfanya mtu kutumia maji bila kuathiri watu wengine.

Alisema sababu nyingine ni kusaidia watu kutumia maji bila kuathiri mazingira pamoja na kuwafanya watumiaji wa maji kutumia kistaarabu na kusababisha huduma hiyo iendelee kuwepo.

Profesa Mkumbo aliwataka Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (Dawasa), kuhakiki na kutambua visima vilivyopo ili viweze kufuata taratibu hizo.

Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji namba 11 ya mwaka 2009 kifungu cha 43(1) ambacho kinamtaka mtu yeyote anayetaka kuchepusha, kukinga, kuhifadhi, kuchukua na kutumia maji kwenye chanzo cha maji juu ya ardhi au kujenga miundombinu yeyote kuomba kibali.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam, Profesa Mkumbo, alisema hadi sasa  kuna maeneo 23 tu ambayo yana shida ya maji na tayari yameshawekewa matanki kwa ajili ya kusaidia uvunaji na usambazaji wa maji.

Katika hatua nyingine, Profesa Mkumbo, amesema Serikali imeanza kujiandaa kuvuna maji ya bahari ili yaweze kutumika katika Jiji la Dar es Salaam baada ya mwaka 2035.

“Mwaka 2030 Jiji la Dar es Salaam linakadiriwa litakuwa na watu milioni kumi, hivyo mahitaji ya maji yatakuwa makubwa, ili kukidhi mahitaji hayo Serikali imejipanga kuvuna maji ya bahari ambayo yatakuwa yanatumika katika jiji hilo lengo ni kuhakikisha tunaondoa adha ya maji,” alisema Profesa Mkumbo.

Kwa upande wa Makonda, alisema hali ya upatikanaji wa maji kwa Jiji la Dar es Salaam kwa sasa ni nzuri na kwamba katika maeneo mablimbali ikiwemo Ilala na Kigamboni asilimia 40 ya wakazi pekee hawana maji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles