25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

JKCI kutimiza malengo yake kupandikiza moyo

 NA VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi, amesema wamebakiza hatua chache kabla ya kuanza kufikia ndoto yao ya kupandikiza moyo nchini.

Pia amesema wamedhamiria kufikia hatua ya kufanya upasuaji huo mkubwa ambao haujawahi kufanyika nchini kwa kuwatibu watu wanaokabiliwa na matatizo ya moyo.

Akizungumza katika mahojiano maalumu yaliyorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kuhusu afya ya moyo, alisema wana matarajio hayo makubwa kwa sababu tangu taasisi hiyo ilipoanzishwa rasmi mwaka 2015 hadi sasa wamefanya aina mbalimbali za upasuaji wa kibingwa kutibu magonjwa ya moyo kwa mafanikio makubwa.

Alitaja miongoni mwa aina za upasuaji zinazowapa nguvu ya kufanya vizuri zaidi siku zijazo ni kuvuna mishipa ya damu kutoka miguuni na kuipandikiza katika moyo ili kuizibua iliyoziba kwa mtu mzima mwenye umri wa miaka 82.

Alitaja upasuaji mwingine ni ule uliofanyika hivi karibuni wa kuzibua mishipa ya moyo ya mtoto mdogo wa wiki mbili iliyokuwa imeziba.

“Tangu mwaka 2016 hadi sasa tumeshawafanyia upasuaji wa kuvuna mishipa ya miguu kutibu moyo jumla ya wagonjwa 66, hawa ni watu wazima na tumeweza pia kuwapandikiza betri wagonjwa 16 ambao utendaji kazi wa mioyo yao ulishuka hadi asilimia 15,” alisema.

Pia alisema tangu mwaka 2015 hadi sasa zaidi ya wagonjwa 200,000 wamepatiwa matibabu katika taasisi hiyo na ikiwa wagonjwa hao wangepelekwa nje ya nchi ingechukua miaka 14 kufikia idadi hiyo.

“Serikali kila mwaka ilikuwa inawapa rufaa kwenda nje kutibiwa takribani wagonjwa 400 na 200 kati yao walikuwa ni wa moyo, kila mmoja aligharimu kiasi cha shilingi milioni 29.

“Tunapotazama mafanikio haya tunaona tumebakiza hatua ndogo kuweza kufanya aina nyingine za upasuaji ambazo kwa sasa nchini hatufanyi ikiwamo ile ya kupandikiza moyo, ipo siku nasi tutafikia huko,” alisema.

Alisema kila siku wanaona wagonjwa 300 katika kliniki zao, wanapokea kwa rufaa wagonjwa wa moyo kutoka nchini Uganda, Kenya, Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kuwatibu.

“Nimekuja hapa Zanzibar kuhudhuria hafla ya kutiliana saini mkataba wa makubaliano kuanza kupokea wagonjwa wa moyo wa rufaa kutoka huku, hatua hii ni ukamilifu katika yale waliyokubaliana mawaziri wa afya wa Bara na Visiwani, wagonjwa wataanza kuletwa JKCI kwa rufaa,” alisema.

Alisema hadi sasa jumla ya wagonjwa 50 wa moyo kutoka Zanzibar wamepatiwa matibabu katika taasisi hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Juma Salum, alisema watoto ndilo kundi linaloonekana kukabiliwa na matatizo mbalimbali ya moyo visiwani humo.

“Kuna tunaowapokea wana matundu kwenye moyo, wengine maumbile ya mishipa imekaa vibaya, wataalamu wetu wakishawachunguza tulikuwa tunawapa rufaa kwenda India au Israel.

“Serikali inalipa gharama kubwa kwa matibabu yao, Julai, 2018 pekee bodi ilichambua ikaainisha wagonjwa 60 ambao 51 walipelekwa nje ya nchi na tisa walipelekwa JKCI kutibiwa,” alisema.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,277FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles