29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAUTAKA MGODI WA URANI KUANZA UZALISHAJI

 Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani

Na VERONICA SIMBA – NAMTUMBO

SERIKILI imeuagiza Mgodi wa Mantra uliopo Namtumbo mkoani Ruvuma, kuanza uzalishaji wa madini ya urani ndani ya miaka miwili kuanzia sasa, ili wananchi waweze kunufaika kama ilivyokusudiwa.

Agizo hilo lilitolewa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, alipotembelea mgodi huo akiwa katika ziara ya kazi mkoani Ruvuma, kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na wizara yake.

Dk. Kalemani alisema kulingana na mpango-kazi uliokuwapo, mgodi huo ilikuwa ufunguliwe ndani ya miezi 24 tangu ulipopatiwa leseni ya uchimbaji, Aprili 5, mwaka 2013, lakini uzalishaji haujaanza hadi sasa.

“Mlipewa miaka miwili ya ujenzi ambayo imeshapita. Huu ni mwaka wa nne sasa, hivyo tunasema anzeni uzalishaji ndani ya miaka miwili ijayo,” alisema.

Akifafanua kuhusu kutoa miaka miwili ili kampuni hiyo iwe imeanza uzalishaji, Dk. Kalemani alieleza kuwa mpango wa kisheria na ule wa ujenzi, miaka miwili imeshapita, hivyo ni haki kwa Serikali kuitaka kampuni hiyo kuanza kuzalisha ili ianze kulipa kodi na kuajiri Watanzania.

Ilielezwa kuwa mgodi huo unaweza kuajiri zaidi ya watu 1,500 katika hatua za mwanzo za ujenzi na zaidi ya watu 2,000 ukianza uzalishaji, jambo ambalo Dk. Kalemani alisema kuwa ni la manufaa kwa Watanzania.

Aidha, alitaja faida nyingine kubwa ya mradi huo kuwa ni mapato kwa Serikali yatakayotokana na ushuru, kodi na tozo mbalimbali ambazo kisheria haziwezi kutozwa ikiwa mradi haujaanza kuzalisha.

“Dhamira yetu ni kupata kodi ili tuijenge nchi yetu kwani bila kodi hakuna Serikali inayoweza kukua kiuchumi. Hivyo tunawahimiza Mantra mfungue mgodi ili muanze kulipa kodi na kuajiri wafanyakazi wengi zaidi ili Watanzania wanufaike,” alisisitiza.

Akizungumzia sababu inayotajwa na wamiliki wa mgodi huo, ya kushuka kwa bei ya madini hayo katika soko la dunia kuwa inachangia kuchelewesha kuanza uzalishaji, Dk. Kalemani alisema kuwa inaweza kuwa kweli, lakini haina uzito wa kufanya uamuzi wa kuacha kuwekeza.

Alisema kupanda na kushuka kwa bei ni jambo la kawaida, hivyo aliutaka uongozi wa Mantra kuhakikisha mgodi unafunguliwa mapema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles