NA LEONARD MANG’OHA, DAR ES SALAAM
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amelaani kitendo cha Mwalimu wa Shule ya Msingi Kiteba mkoani Kagera, Respicius Patrick (50), kumpiga na mwanafunzi wake wa darasa la tano, Siperius Eradius na kumsababishia kifo.
Alikuwa akizungumza Dar es Salaam jana baada ya kufungua kongamano la tano la kuangalia namna ya kuboresha ufundishaji wa somo la hesabu lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Aga Khan.
Profesa Ndalichako alisema kitendo cha mwalimu huyo kinaweza kutisha wazazi wakasita kuwaruhusu watoto wao kwenda shule.
“Ni kitendo ambacho hakiakisi matakwa ya Serikali na ni kitendo ambacho kiko kinyume na malengo ya serikali.
“Hivi sasa imeboresha elimu na inafanya kazi kubwa katika kuhakikisha watoto wote wanapata elimu.
“Lengo la Serikali ni kutoa elimu bure siyo kuwafanya watoto waende shule wakiwa na shaka, kwa hiyo naomba niwahakikishie wananchi kuwa Serikali inalichukulia jambo hilo kwa uzito.
“Nimekwishaongea na Mkuu wa Mkoa ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na niombe kuwe na amani na utulivu katika kipindi ambacho Serikali inafanya kazi yake” alisema Profesa Ndalichako.
Waziri aliwataka wananchi kutambua kuwa mwalimu aliyetekeleza tukio hilo hakutumwa na Serikali kufanya yale aliyoyafanya.
Aliwahakikishia wananchi kuwa shule ni sehemu iliyo salama kwa hiyo asitokee mtu akafanya vitendo ambavyo hata wazazi watakuwa wanafikiria kuwaruhusu watoto kwenda shule au wasiende.
“Kama Serikali tutaendelea kulinda na kuchukua hatua kwa mtu yeyote kwa namna yoyote ile anayoweza kufanya wazazi au watoto waone kuwa shule siyo mahali salama.
“Kwa hiyo naomba sana Watanzania katika kipindi hiki viachiwe vyombo vifanye kazi yake,” alisema Profesa Ndalichako.
Aliongeza kuwa alitegemea kwa umri wa mwalimu aliyetenda kosa hili yeye ndiye angekuwa anawasadia walimu vijana jinsi gani wafanye kazi yao
“Ni bahati mbaya imetokea, lakini bahati mbaya hiyo isije ikatafsiriwa kuwa shule siyo mahali salama.
“Shule ni mahali salama kabisa na yeyote yule ambaye anatishia usalama wa watoto shuleni serikali itamshughulikia kwa nguvu zake zote,” aliongeza Profesa Ndalichako.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, juzi aliwaambia waandishi wa habari kuwa mwanafunzi huyo alipigwa na mwalimu wake baada ya kupokea mzigo wa mwalimu wak,e Herieth Gerald (46), na baadaye kutuhumiwa kuiba Sh 75,000, kitambulisho cha mpiga kura, kitambulisho cha uraia na simu ya mkononi.
Wakati huohuo, Profesa Ndalichako akizungumza wakati wa kufungua kongamano la hesabu, alisema: “Kumekuwa na changamoto katika kufundisha hesabu.
“Asilimia kubwa ya wanafunzi wamekuwa hawafanyi vizuri na hii siyo kwa Tanzania tu, somo la hesabu ni karibu nchi nyingi kumekuwa na matatizo”.
Alisema katika kongamano hilo wataalamu hao wa hesabu watangalia ni namna gani mwalimu ataweza kutumia mifano inayoendana na mazingira ya nchi husika kumwezesha mwanafunzi kuona kuwa hesabu ni kitu anachoishi nacho katika maisha ya kila siku katika jamii yake.
Profesa Ndalichako alisema pia taangaliwa ni kwa namna gani walimu wanawahamasisha wanafunzi kupenda somo la hesabu na jitihada za wanazozichukua kuwafanya wanafunzi wapende hesabu na kutambua jukumu lao katika kuhakikisha wanafunzi wanapenda somo hilo.
Mkuu wa Chuo cha Kikuu cha Aga Khan, Profesa Joe Lugalla, alisema wameamua kufadhili kongamano hilo kusaidia kuboresha elimu nchini hasa katika somo hilo ambalo ufundishaji wake katika shule za msingi za sekondari umekuwa tatizo.
“Si kwamba watoto hawana akili, ila walimu wengi hawajui kufundisha watoto walipende.
“Kwa hiyo katika masomo yetu tunayoyatoa katika ngazi ya masters (shahada ya pili) moja ya masomo tunayofundisha ni namna bora ya kufundisha hesabu,” alisema Profesa Lugalla.