Na RAAMADHAN HASSAN -DODOMA
SERIKALI ya Tanzania imesaini mikataba miwili ya msaada na Serikali ya Uswisi yenye thamani ya Sh bilion 44.1 kwa ajili ya kugharamia Mpango wa Awamu ya Pili wa kunusuru Kaya Maskini (Tasaf) na Mfuko pamoja wa Afya kwa Mwaka wa Fedha 2020-2021.
Akizungumza na waandishi wa Habari jana jijini hapa wakati wakutiliana saini mikataba hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James alisema Sh. bilioni 39.15 ni kwa ajili ya kugharamia awamu ya pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (Tasaf).
Alisema shilingi bilioni 4.95 ni kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa pamoja wa Afya kwa mwaka wa Fedha 2020/2021.
“Ushirikiano wa kimaendeleo baina ya nchi hizi mbili utazidi kuimarika tupo nao tokea miaka ya 1960 ambayo imethibitishwa na miradi inayoendelea, iliyofadhiliwa na Serikali ya Uswisi ikiwemo misaada miwili tuliyopokea,”alisema Katibu Mkuu huyo.
Alisema mpango wa kunusuru Kaya Maskini awamu ya kwanza ulitekelezwa kwa kipindi cha kwanza mwaka 2013 hadi Desemba 2019 ambapo utekelezaji ulilenga mamlaka za serikali za mitaa 159 Bara na Visiwani.
Vilevile,Katibu Mkuu huyo alisema mwaka 2015 kurudi nyuma Hospital za Halmashauri zilikuwa 77 lakini kuanzia mwaka 2015 mpaka 2020 zimeongezeka Hospitali 101 hivyo jumla kuwa 178 sawa na ongezeko la asilimia 131.2.
Alisema mwaka 2015 kurudi nyuma kulikuwa na vituo vya afya 718 ambapo alidai mwaka 2015 hadi 2020 vimeongezeka vituo vya afya 487 na hivyo jumla kuwa 1205 sawa na asilimia 67.8.
Katibu Mkuu huyo wa Fedha na Mipango alisema mwaka 2015 kulikuwa na Zahanati 6044 ambapo mwaka 2015 hadi 2020 vimeongezeka 1198 ambapo jumla vimekuwa 7242.
Alisema bajeti ya dawa kwa mwaka 2015 ilikuwa shilingi bilioni 31 kwa mwaka ambapo kwa sasa bajeti ni shilingi bilioni 270 sawa na ongezeko la asilimia 71.0.
“Safari za wagonjwa kwenda Nje ya Nchi kwa mwaka 2015 zilikuwa 683 ambapo tangu awamu ya tano mwaka 2015 hadi 2020 ni safari 64 tu zimefanyika ambapo ni sawa na asilimia 90,kwa sasa wengi wanatibiwa hapa hapa nchini,” alisema.
Kwa upande wake,Balozi wa Uswisi nchini,Didier Chassot alisema Uswisi na Tanzania zimekuwa na mahusiano mazuri ya kidiplomasia na ya muda mrefu ambayo yalianza mwaka 1966.
“Wakati tunaipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kiuchumi na kusababisha ubora wa hali ya maisha ya watu wengi, ni lazima tulinde maisha ya wale ambao hawajafaidika na ukuaji huu hivyo Serikali ya Uswisi inaunga mkono agenda ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu ya kutomwacha yeyote nyuma.
“Hivyo basi leo (jana) tunarasimisha pia mchango mpya wa Dola za Kimarekani milioni 17 fedha hizi zitatumika kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo,”alisema Balozi Chassot.
Balozi Chassot alisema ana imani kwamba kwa pamoja wataweza kufanikiwa zaidi na kuendelea kukuza na kuimarisha uhusiano kati ya Nchi hizo.
Kwa upande wake,Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Ikulu, Dk Moses Kusiluka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) aliishukuru Serikali ya Uswisi kwa msaada huo huku akiahidi kwamba Serikali ya Tanzania itahakikisha unawafikia walengwa.
“Kwa niaba ya walengwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunashukuru kwa msaada huu,tunaahidi fedha hizi zitatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa,”alisema Dk.Kusiluka.