23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatia mguu mgogoro wa wanafamilia kuhusu jengo la urithi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mabinti watano wa familia moja wameingia kwenye mgogoro na kaka yao anayedaiwa kutaka kuwadhulumu mali ya urithi ambayo jingo lililopo Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Jengo hilo linalotumiwa na wapangaji, limekuwa chini ya udhibiti wa kaka huyo, Arafat Bahashwani anadaiwa amekuwa akichukua kodi za wapangaji bila kuwashirikisha wamiliki halali wa mali hiyo.

Inaelezwa jengo hilo ambalo lipo katika kiwanja namba 1 block A kilichopo Kariakoo, lilinunuliwa mwaka 1971 na marehemu baba yao, Abdallah Bahashwani kwa ajili ya biashara na mwaka 1996 alihamisha umiliki kutoka kwake kwenda kwa watoto wake watano wa kike.

Tayari sehemu ya jengo hilo imebomolewa na inadaiwa Arafat anataka kujenga jengo jingine, jambo ambalo amelifanya bila kuwashirikisha wamiliki hao.

Mgogoro huo umekua na kuisukuma Serikali kuingilia kati ambapo Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, Shukrani Kyando ametembelea jengo hilo leo Jumatatu Julai 15, 2024 na kuandaa kikao na wapangaji, ili kufahamu kuhusu mmiliki halali.

Akizungumzia mgogoro huo, mmoja wa wamiliki, Saada Bahashwani amesema jengo hilo lilinunuliwa na marehemu baba yao mwaka 1971 na kote kulikuwa na wapangaji na familia zao.

Amedai oda ya kubomoa jengo hilo imetolewa na Arafat ndiye anayesimamia mchakato huo, akitaka kujenga jengo jingine kwenye mali si yake, hivyo ameiomba Serikali kuwasaidia kupata haki yao ili waendeleze.

“Hii ni mali yetu watoto wa kike, tunataka tuiweke kwenye hali ya watu kuishi kwa amani, wapangaji wasikerwe, kila siku kubandikiwa notice (taarifa) waondoke, watu wameshalipa kodi humu ndani.

“Kuna mpangaji ametoka kulipa Sh milioni 15 juzi tu, baada ya wiki anaona notice mlangoni kwake, ana kamera dukani kwake, saa nane za usiku anaona watu wanabadika notice. Kama ni kitu cha halali, kwanini aje kuweka usiku?” amehoji Saada.

Saada amesema atakuwa tayari kuzungumza na wapangaji na kuwekeana utaratibu, kwani walikuwa hawajui ukweli kuhusu umiliki wa jengo hilo, hivyo wawe na amani na wale waliolipa kodi zao pia watazingatiwa

Mgogoro wa ardhi na nyumba baina ya wanafamilia hao umechukua sura mpya baada ya Serikali kuingilia kati na kuwatambua wanawake hao kama wamiliki halali wa nyumba hiyo waliyodhulumiwa na kaka yao.

Akizungumzia mgogoro huo, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, Shukrani Kyando amesema anautambua mgogoro huo wa kiwanja namba 1 block A na wanawake hao waliwahi kwenda ofisini kwake kulalamika.

Amesema mwaka 1996, baba yao aliridhia kuhamisha mali hiyo kutoka kwake kwenda kwa watoto wake watano na kwamba watoto hao ndiyo wapo kwenye daftari la Msajili wa Hati na Nyaraka kama wamiliki wa jengo hilo.

“Jambo lolote litakalofanyika kwenye hili jengo ni lazima liridhiwe na wamiliki, ni lazima liamriwe na wamiliki. Tangu mwaka 1996 hadi sasa, hawa watano wamekuwa kwenye mgogoro na kaka yao anayeingilia mali za hawa,” amesema.

Kyando amewaita ofisini kwake wapangaji wa jengo hilo ili kuwafafanulia ukweli kuhusu umiliki wa jengo hilo kwani inawezekana wamedanganywa. Baada ya kuwaeleza ukweli, amesema watawajibika kulipa kodi na mambo mengine kwa wamiliki hao watano wanaotambulika.

Alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia mgogoro huo, Arafat hakupokea simu yake na hata alipotumiwa ujumbe, hakujibu chochote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles