28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yataka uwekezaji zaidi mafunzo ya bima

Na Mwandishi Wetu, Unguja

Changamoto za upatikanaji wa huduma muafaka za bima nchini zitapata ufumbuzi kutokana na uwepo na wataamu wenye mafunzo stahiki kwa ajili ya kuzifanyia kazi na kusaidia maendeleo ya sekta hiyo kwa ujumla.

Hiyo ni kwa mujibu wa Kamishna wa Bima, Dk. Mussa Juma, ambaye amewataka watoa huduma hizo wote kuwekeza zaidi katika mafunzo na elimu ya bima kwa wafanyakazi wao ili waweze kulihudumia soko kikamilifu na kusaidia kubuni bidhaa zinazoendana na mahitaji ya taifa na mazingira ya nchi yetu.

Akiongea mwishoni mwa wiki wakati wa mafunzo ya maafisa bima wa Benki ya NMB, Dk. Juma alisema uwekezaji huo utayasaidia makampuni ya bima, benki zinazofanya biashara hiyo, mawakala na wadau wengine kuwa na wafanyakazi wenye sifa za kitaaluma katika tasnia hiyo.

Alisema kada hiyo ya wataalamu ni muhimu si tu katika kurahisisha ukataji wa bima na upatikanaji wake bali pia kwenye kusaidia kuwepo kwa bidhaa sahihi sokoni pamoja na kuongeza uwezo wa kuwahudumia wananch. Pia watashiriki kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo mchango mdogo kwenye uchumi na maendeleo ya nchi, alifafanua kiongozi huyo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).

“Sheria ya Bima inataka kila mtoa bima, awe benki au hata wakala yeyote wa bima, anatakiwa kufanya mafunzo kwa watoa huduma wake. Nawapongeza NMB kwa kuzingatia hilo na sisi kama wasimamizi tutahakikisha mnapata msaada mnaotaka ili kusogezahuduma za bima kwa Watanzania wengi zaidi.

“Kuingia kwa Benki ya NMB kwenye bancassurance ni ushindi mkubwa kwa sisi tulioko kwenye sekta ya bima nchini, kwani tayari kwa miezi michache tu tumeshaanza kuona mabadiriko ya utoaji huduma pia watu wengi wamepata ahueni kwani Benki ya NMB imesambaa kila kona ya nchi hii, bara na hapa Zanzibar,” alisema Dk Juma katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoanza Ijumaa.

Taasisi hiyo kubwa ya fedha nchini ilianza kutoa huduma za bima Februari, mwaka huu ikiwa ni benki ya kwanza kuanza rasmi kufanya biashara hiyo ijulikanayo kitaaluma kama bancassurance.

Kwa mujibu wa, Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa NMB, Emmanuel Akoonay, uwekezaji katika mafunzo ya wafanyakazi wa kitengo cha bima umekuwa wa tija kubwa kwa benki hiyo na upatikanaji wa huduma zake.

Alisema lengo la kuzindua kitengo cha NMB Bancassurance lilikuwa ni kusaidia kuleta huduma za bima karibu zaidi na Watanzania kwani watu wengi walikuwa hawafikiwa na huduma hizo.  Hilo limefanikiwa kwani watu wengi sasa wanatumia matawi zaidi ya 225 ya NMB na mawakala zaidi ya 8,000 kukata bima hata walio vijijini na maeneo ya pembezoni kabisa huku wengi zaidi wakitarajiwa kuhudumiwa kidijitali, Akoonay alifafanua na kuongeza:

“Tangu kuzinduliwa kwa bancassurance, zaidi ya wafanyakazi 250 wamekwishapokea mafunzo haya na kupewa vyeti. Mafunzo haya yameongeza sana utoaji huduma na hivyo kuwa na wastani wa watu zaidi ya 30,000 wanaokata bima kila mwezi kupitia NMB.

“Mipango yetu ikishakamilika ya kuanza kutoa huduma za bima kidijitali ikiwemo kupitia NMB Mkononi, watu wengi zaidi wataweza kupata huduma za bima popote pale walipo na wakati wowote na hivyo kutoa kabisa changamoto ya umbali katika kufuata huduma za bima.”alisema Akoonay.

Pia, Akoonay alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wafanyakazi wao ili kuendana na mabadiriko yanayotokea sokoni na hivyo kutengeneza timu yenye uelewa wa juu katika sekta ya bima.

Naye Afisa Mwandamizi wa Bima NMB, Martine Massawe, alisema baada ya mafunzo hayo washiriki wataweza kuyafahamu mahitaji ya soko la bima na kuyashughulikia kwa weledi mkubwa. Baada ya kujua kinachoendelea sokoni kupitia mafunzo mbalimbali, wafanyakazi wa NMB wataiwezesha benki hiyo kuwa mshindani mzuri sokoni.

Katika mafunzo hayo, mwezeshaji Mkuu wa mafunzo hayo yaliyowashirikisha pia viongozi na wataalamu kutoka makampuni ya bima yanayoshirikiana na NMB alikuwa aliyekuwa Kamishna wa TIRA, Dk. Baghayo Saqware.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles