ASHA BANI-DAR ES SALAAM
SERIKALI imesitisha kutoa vibali vya uagizaji sukari nje ya nchi kwa makampuni yanayozalisha bidhaa hiyo na badala yake itaruhusu makampuni yasiyozalisha kufanya hivyo.
Akizungumza jana Dar es Salaam katika mkutano na wadau wa sekta binafsi na wa kilimo, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema lengo la kufanya hivyo ni kutaka makampuni yanayojihusisha na uzalishaji kuendelea kuongeza nguvu katika uzalishaji na si kama ilivyo sasa nguvu zaidi wameweka katika kuagiza nje ya nchi.
Alisema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuepukana na uhaba wa sukari ambao unaweza kulikumba taifa katika siku zijazo na kusababisha kero kwa walaji kutokana na kuadimika kwake.
Akizungumzia akiba iliyopo nchini kwa sasa, alisema itatosha hadi kufikia Mei, lakini kuanzia Juni na kuendelea kuna haja ya Serikali kuruhusu makampuni mengine kuagiza tani 28,000 ziingizwe ili kufidia pengo hilo.
“Kwa sasa tumekaa na kufanya vikao, tumeona uagizwaji wa sukari nje ya nchi unaofanywa na wazalishaji wa sukari umekua kwa kasi kuliko hata kuzalisha, sasa tukifanya hivi viwanda vyetu vitakuwa havizalishi.
“Na badala yake tutapoteza fedha nyingi katika kuagiza badala ya sisi wenyewe kuwa wazalishaji, hivyo kutakuwa na utaratibu maalumu kwa makampuni mengine kupewa vibali vya kuagiza,’’ alisema.
Alisema tatizo jingine ni wazalishaji wa hapa nchini hawaweki nguvu katika kuongeza nguvu hata ya kununua mitambo, kulima miwa na badala yake nguvu iko kwenye kuagiza tu.
“Na hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu kutakuwa na upungufu wa tani 22,000. Sisi tunahitaji kuwa na ziada, hivyo Serikali kwa utaratibu wake tunaangalia uwezekano kuagiza tani 28,000 hadi 30,000 hivyo mwezi Juni tunatakiwa kuwa tumejiandaa kweli kweli,’’ alisema Hasunga.
Alisema hadi sasa kuna uhitaji wa sukari tani 670,000 zilizopo 300,000 zitakidhi hadi Mei, hivyo Serikali kwa kutumia utaratibu mwingine itaagiza tani 25,000 hadi 28,000.