27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Serikali yasisitiza Umoja na Amani kwa kufuata Sera za Rais Samia

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Serikali imeeleza kuwa umoja na amani nchini Tanzania vitaendelea kuimarika ikiwa vyama vyote vya siasa vitafuata falsafa ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inayolenga maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko, na ujenzi upya wa taifa. Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kujitambulisha kwenye vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Oktoba 8, 2024, jijini Dar es Salaam.

“Wanasiasa ndio kila kitu kwa wananchi, hivyo endeleeni kutunza amani hii ili Tanzania iendelee kusonga mbele kwa kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli. Umoja na amani ndio unaosababisha viongozi wa serikali kutembelea vyama vya siasa na kufanya mambo mengi ya kimaendeleo ndani ya nchi,” alisema Lukuvi.

Akiangazia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ujao, Lukuvi alibainisha kuwa Rais Dk. Samia amesisitiza chaguzi hizo ziwe za uhuru, heshima, na haki kwa faida ya Watanzania wote.

“Nawahakikishieni kuwa uchaguzi wa mwaka huu utaenda vizuri kwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa. Katika mashindano yoyote, ni lazima kuwepo na ushindani, hivyo hata uchaguzi wa mwaka huu na mwaka ujao mshindi lazima atapatikana bila kujali anatoka chama gani,” alieleza Lukuvi.

Alivitaka vyama vya siasa nchini kuacha siasa za mihemko na badala yake kufanya siasa zenye hoja na maelewano, akisema kuwa Rais Dk. Samia amesisitiza chaguzi za mwaka huu ziwe na utulivu na ziwe mfano wa kuigwa.

Viongozi wa vyama vya siasa waliozungumza baada ya ziara hiyo waliihakikishia Serikali kuwa watashiriki katika uchaguzi kwa utulivu na nia ya kulinda amani ya nchi. Mwenyekiti wa United Democratic Party (UDP), John Cheyo, alisema, “Sera yetu kubwa ni upendo, na tunajua kuwa siasa si uadui. Tutahakikisha falsafa za Rais Dk. Samia zinatuongoza vyema.”

Makamu Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini, alisema chama chake kimejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu na kuhamasisha wanachama wake kujiandikisha katika daftari la wapiga kura linalotarajiwa kuanza Novemba 11, 2024.

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alishukuru Serikali kwa kuanzisha falsafa ya 4R, akisema kuwa imeleta mabadiliko makubwa ndani ya sekta ya siasa. “Naona 4R zimeshaanza kufanya kazi yake. Leo hii Waziri anatembelea vyama vya siasa ofisini kwao, hayo ni mabadiliko makubwa,” alisema Lipumba.

Waziri Lukuvi ameanza ziara hiyo ya kutembelea vyama vya siasa Oktoba 7, ambapo amevitembelea vyama vya CUF, UDP, NCCR-Mageuzi, na NLD. Jumla ya vyama 19 vyenye usajili wa kudumu vinatarajiwa kutembelewa katika ziara hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles