25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Serikali yamkataa Mkurugenzi wa Bugando0

Hospitali ya Bugando
Hospitali ya Bugando

NA FREDERICK KATULANDA, MWANZA

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imemkataa mkurugenzi mpya wa Hospitali ya Rufaa Bugando, Dk. Kien Mteta, aliyeteuliwa na kanisa hilo kushika nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Profesa Charles Majinge.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imelazimika kuliandikia barua kanisa hilo kueleza jinsi isivyotambua mabadiliko hayo yaliyofanywa kinyume cha mkataba uliopo kati yake na kanisa hilo.
Taarifa hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo, alipokuwa akizungumza na MTANZANIA Jumatatu kwa simu.

Pallangyo alitoa msimamo huo baada ya kutakiwa na MTANZANIA Jumatatu, aeleze msimamo wa Serikali baada ya kanisa hilo kusitisha mkataba wa Profesa Majinge kinyume cha utaratibu.

“Tayari tumeshawaandikia barua Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), kuwafahamisha jinsi walivyovunja mkataba na tumewaeleza jinsi tusivyomtambua mrithi wa mkurugenzi aliyetimuliwa.

“Sisi kama Serikali, bado tunatambua mkataba wa Profesa Majinge na kama kanisa lilikuwa linataka kumpata mkurugenzi mwingine lilipaswa kufuata utaratibu badala ya huu waliouchukua.

“Kabla ya kuwaandikia barua ya kupinga uamuzi wao, tulipokea barua kutoka TEC ikituarifu kuwa wamempata mkurugenzi mpya ambaye anatoka KCMC.

“Tulipopata barua hiyo tulishtuka kwa sababu makubaliano yalikuwa yamekiukwa, kwa hiyo tukawaandikia barua tukiwakumbusha wazingatie mkataba uliopo huku tukiwaambia wazingatie mkataba wa makubaliano (MoU), lakini pia tuliwakumbusha kwamba, mkataba wa ajira wa Profesa Majinge, unamalizika Julai mwaka 2016 na si vinginevyo,” alisema Pallangyo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumatatu wiki iliyopita, Profesa Majinge alithibitisha kuondolewa kazini na kueleza kuwa tayari ameshakabidhi ofisi baada ya kupokea barua iliyokuwa ikimtaka kufanya hivyo.

“Nimeondoka kazini, nisingependa kuzungumzia masuala haya na kama una chochote, hebu waulize wahusika ila kwa kifupi nimeondolewa hapo na sababu sijajua kwani nilielezwa nikabidhi ofisi japokuwa mkataba ulikuwa bado,” alisema Profesa Majinge.

Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa za ndani zilidokeza kuwa kuondolewa kwa mkurugenzi huyo, kunadaiwa ni kutokana na kushindwa kuwasilisha sehemu ya fedha za mapato ya ndani ya hospitali hiyo kwa ajili ya kuchangia Benki ya Mkombozi inayomilikiwa na Kanisa Katoliki nchini.

Mkataba wa Kanisa na Serikali

Katika makubaliano baina ya Serikali na Kanisa Katoliki, Serikali ndiyo yenye jukumu la kutoa mkurugenzi wa hospitali hiyo. Kwa maana hiyo, Profesa Majinge alikuwa ni mwajiriwa wa Serikali aliyekuwa na mkataba wa kuongoza hospitali hiyo hadi mwaka 2016.

Mkataba huo ambao ulisainiwa Oktoba 23 mwaka 1985 baina ya Serikali na Kanisa Katoliki kupitia bodi ya wadhamini kwa niaba ya TEC, katika kifungu cha 6 (b) unaeleza kuwa, nafasi ya mkurugenzi ambaye ndiye atakuwa mtendaji mkuu wa taasisi hiyo, atapendekezwa na Bodi ya Uteuzi ya TEC baada ya kushauriana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Mchakato wa kumtoa mkurugenzi

Kwa mujibu wa barua yenye kumbukumbu namba TEC/PR/1/340 ya Julai 2013 iliyoandikwa na Rais wa TEC, Mhashamu Askofu, Tarcius Ngalalekumtwa kwenda Ofisi ya Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Profesa Majinge aliombwa kujiandaa kuachia ngazi ifikapo Julai 2014 ingawa mwajiri wake ambaye ni Serikali hakupewa nakala ya barua hiyo.

Katika barua hiyo ambayo nakala yake tunayo, Mhashamu Askofu Ngalalekumtwa anaeleza kuwa, TEC walikuwa wakitafuta mkurugenzi mpya ambaye walikuwa wakitarajia kumpata Januari 2014.

Pamoja na mkurugenzi huyo mpya kupatikana, barua hiyo inasema angelazimika kukaa hospitalini hapo kwa miezi sita akitambulishwa masuala mbalimbali ya kiutawala hadi mwishoni mwa mwezi Juni 2014.

“Mtu huyo atafanya kazi nawe katika kipindi cha miezi sita mpaka mwishoni mwa Juni 2014 na katika wiki ya kwanza ya Julai 2014, utapaswa kuondoka,” ilieleza sehemu ya barua hiyo ya Rais wa TEC ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Iringa.

Sambamba na barua hiyo, TEC iliunda kamati maalumu iliyopewa jukumu la kumtafuta mkurugenzi mpya ambaye angeweza kuongoza hospitali hiyo na pia kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Bugando (CUHAS). Kamati hiyo ilifika Hospitali ya Bugando, Oktoba 8, 2013 na kuzungumza na wafanyakazi.

Kamati hiyo iliyotambulika kama Search Team (Timu ya Utafiti), iliongozwa na Padri Dk. Charles Kitima, aliyewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustino (SAUT) na ilikuwa na wajumbe kadhaa wakiwamo, Dk. Frederick Kigadye pamoja na Profesa Peleka kutoka chuo kimoja cha nchini Marekani.

Kitendo cha TEC kuchukua uamuzi wa kusitisha mkataba wa Profesa Majinge, kilianza kuandaliwa mapema baada ya Serikali kuamua kumuongezea mfanyakazi huyo muda wa miaka mitatu kuendelea kuiongoza asasi hiyo.

Serikali kupitia Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Machi 5, 2013 ilitoa kibali cha ajira ya mikataba kwa kipindi cha miaka miwili kwa maofisa tisa na ofisa mmoja ambaye ni Profesa Majinge, alipewa miaka mitatu.

Wafanyakazi wamwombea muda

Taarifa za kuondolewa kwa Profesa Majinge zilishtua wafanyakazi wa hospitali hiyo ambapo kupitia Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE), Tawi la Bugando, waliamua kumuandikia barua Askofu Ngalalekumtwa, wakiomba amruhusu mtumishi huyo aendelee kuwapo hospitalini hapo hadi mkataba wake utakapomalizika.

Barua hiyo yenye kumbukumbu namba T50/140 ya Oktoba 15, 2013 ilisainiwa na Mwenyekiti wa TUGHE, Tawi la Bugando P. Bachuba na Katibu wake, D. Misinzo.

Viongozi hao walieleza umuhimu wa Profesa Majinge kuendelea kuwapo hospitalini hapo kuwa ni pamoja na kuendelea kusimamia miradi mbalimbali ikiwamo uanzishaji wa vitengo vya dharura, maboresho ya kitengo cha afya ya akili, kitengo cha upasuaji wa moyo, upasuaji wa kichwa na mfumo wa ufahamu pamoja na usimamizi wa majengo ya saratani, upasuaji na jengo la Bima ya Afya ya Taifa.

Katika barua yao hiyo, TUGHE walisema Profesa Majinge anatakiwa kuendelea kusimamia kuanzishwa kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya hospitali kwa vile yeye ni kiungo muhimu kwa wahisani wa ndani na nje ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

6 COMMENTS

    • Hapa ndiyo unapoona tofauti ya mwandishi makini na mwandishi kajaja. Hii ni mara ya pili Katulanda unaandika habari hii lakini uleti habari za upande wa pili wa TEC kuhusu mtu huyu anayeitwa Prof Majinge ( to me is not even a professor, 2 publication, you become a professor where exactly on earth in academic environment?). Anyway forget about this.
      Katulanda ukiangalia ndani ya habari yako, wewe na Prof Majinge na Katibu wa wizara mnajichanganya tu. Hili uwe mkurungezi lazima upendekezwe na TEC na upeleke barua ya TEC wizara ya Afya na ustawi wa jamii hili upitishwe na kulipwa mshahara. Sasa Katulanda jiulize hivi, mkataba ni wa miaka mitatu mitatu na unaweza kurudiwa (re-newable upon satisfactory performance in the first contract). Sasa imekuaje serikali ikampa mkataba wa kuanzia 2013-2016, wakati huo huo TEC ulishampa barua ya kutokuingia naye mkataba mpya kuanzia 2013? Muulize katibu wa wizara, ilikuaje akampe mkataba mpya wa kazi (2013/2016) wakati hana barua ya uthibitisho wa barua toka TEC inyothibitisha kumuongezea muda wa kuwa mkurugenzi mpaka 2016? Na kama nayo hii barua toka TEC, ilikuwaje tena aliyetoa uthibitisho wa kuendelea na ajira yake, yaani TEC chini ya Askofu Ngalelekumtwa,ambayo katibu wa wizara aliitumia kumpa mkataba mpya ageuke tena na kumpa narua ya TEC kutokuwa tayari kuendelea na huduma ya Dr. Majinge hapo BMC?
      Katulanda na Dr. Majinge jiulizeni haya maswali kabla ya kuandika lawana zenu kwa umma. Dr. Majinge, you are only looking for public sympathy which you will not get anyway. What goes around comes back. I think you remember well when 1kg of beef turned to be a 500kg of beef from that women

  1. Katika maisha yangu sijawahi kuona mkurugenzi mpenda majungu asiyependa maendeleo ya watu,mzinzi(kwa maana amekuwa kitembea na wafanyakazi wake ofisini kwake na kwingineko(Ushaidi ninao) kwa ahadi za kuwapa pesa magari na kuwapa vyeo,nepotist(anawapa ndugu zake nafasi) kama huyu mbaya zaidi inasemekana kwamba amefoji saini ya mwenyekiti wa baraza la maaskofu ili aweze kupata Baraka za serikali kwenye mkataba unaosemwa(2013-2016). Mbaya zaidi kulipa waandishi wa habari ili habari hii ikae inarudiwa rudiwa ni kuonesha harufu mbaya ya rushwa,na kwa taarifa yenu extensive audit ikifanyika mtaona uvundo aliofanya.Prof Jinge JIREKEBISHE,huwezi kuwakandamiza watu milele!!!Kama ana ushahidi wa madai yake aende baraza la usuluhishi wa migogoro kazini atasikilizwa!!Nomba kuwasilisha.

  2. Sabubu zilizotolewa na upande wa utetezi kwamba ameshindwa kuchangia Benki ya mkombozi hazina mashiko watu wenye akili tungependa kujua sakata hili mwanzo mwisho na kama serikali kumuongezea mkurugenzi huyo mkataba wa miaka mitatu utaratibu ulifuatwa. Huenda msuguano ulianzia hapo hatuitaji ubabe katika hili tunahitaji majibu ya kisayansi ili kuokoa hospitali hiyo ambayo ni ya pili ya ukubwa nchini.

  3. Prof. Jinge, TEC sio vipofu kuchukua maamuzi hayo, na hata serikali ijaribu kufanya uchunguzi, kwani nchi yetu watu wamezidi ubadhirifu wa mali za watu. Na mwandishi hatuoni maelezo mengine ya TEC, tunaona maelezo ya Serikali tu, tunaomba maamuzi yafanyike haraka ili kuokoa hospitali hiyo, isiwe kwenye matatizo kwa muda mrefu bila uongozi kwa ajili ya kumtetea mtu mmoja, ambaye pengine ana makosa au hana kosa, mambo yawekwe wazi mapema, ili kama anaendelea au la, kuliko kupoteza muda kujadili mambo yaliyo wazi kabisa. Tunaomba sakata hilo liishe, tunaipenda hospitali yetu, na tunapenda maendeleo, na watu walio na moyo wa upendo na nidhamu katika majukumu yao.

  4. UTATATIBU UFUATWE ILI HOSPITALI IRUDI KWENYE HALI YAKE KAMA ALIVYOKUWEPO PROFESA.
    By the way….. HIVI KATIKA HALI YA KAWAIDA KWA MSOMI TENA PROFESA ANAWEZA KULIPA WATU ILI WAMWANDIKE VIBAYA??
    Hata kama Kanisa lilikuwa halihitaji huduma yake, je Utaratibu umefuatwa?
    Yeye mwenyewe hajalalamika kwa mujibu wa Habari hii, hayo matuhuma mnayosema ni dhana tu, kama yanaukweli mbona hamkuwahi kuyasema?
    *EVERY THING WILL BE OUT OF STOCK NA HAPO NDIO TUTAJUA….

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles