28.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YALIFUNGIA GAZETI LA MWANAHALISI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


SERIKALI imelifungia gazeti la Mwanahalisi kwa kipindi cha miaka miwili kwa kudaiwa kukiuka misingi na sheria za taaluma ya uandishi wa habari.

Akizungumza jana Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, alisema zuio hilo pia linahusu toleo la mtandaoni la gazeti hilo.

Alisema uamuzi huo umechukuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 59 cha Sheria za Huduma ya Habari ya mwaka 2016 baada ya jitihada za muda mrefu za kuwakumbusha wahariri wa gazeti hilo wajibu wa kufuata misingi ya taaluma bila mafanikio.

“Wahariri na uongozi mzima wa Gazeti la Mwanahalisi hawako tayari kufuata maadili ya taaluma hii. Kufungiwa kwa gazeti hili ni juhudi ya mwisho ya serikali kuwataka wabadilike,” alisema Dk. Abbasi.

Alizitaja habari zilizokiuka maadili, uchochezi na kusababisha hatari kwa usalama wa Taifa kuwa ni ya gazeti la Januari 30 hadi Februari 5 mwaka huu iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Ufisadi ndani ya Ofisi ya JPM’, Mwakyembe: Maisha yangu yako hatarini (Aprili 17 – 23) na Makinikia yakwama (Septemba 4 – 10).

Zingine ni ‘Mkuu wa Wilaya ya Karagwe anachafua kazi ya Magufuli’ (Septemba 4 – 10) na Tumwombee Magufuli au Tundu Lissu ya Septemba 18 – 24.

Kwa mujibu wa Dk. Abbasi habari hiyo ilikuwa ya kutunga na ya kuokoteza kejeli za mitandaoni na kwamba ilikuwa na nia ovu na uchochezi dhidi ya Rais na serikali.

“Habari iliyosomeka makinikia yakwama haikuwa na ukweli wowote na ilikuwa na nia ovu ya kuuaminisha umma kuwa mazungumzo hayo yamekwama na kubeza juhudi za Serikali katika kupigania wananchi kufaidika na rasilimali za madini,” alisema.

Alisema kifungu cha 19 (3a – b) cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kisiasa na Kiraia wa mwaka 1966, kinasisitiza kuwa wanataaluma ya habari wana wajibu wa kutokashifu watu wengine, kutoingilia faragha zao, kutoathiri usalama wa Taifa na ustawi wa jamii.

“Tumetumia mbinu zetu zote kama walezi wa taaluma hii na tumejaribu kuwalea tangu Februari mwaka huu, lakini wahariri wa Mwanahalisi walichagua kwa makusudi kutotekeleza wajibu wao.

“Tutaendelea kuchukua hatua kwa wale wanaodhani kwamba uandishi wa habari ni kuandika chochote,” alisema Dk. Abbasi.

 

JUKWAA LA WAHARIRI

 

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limelaani hatua hiyo na kusema kuwa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 inatoa mwanya wa masuala yanayohusu vyombo vya habari kupelekwa mahakamani na kutolewa uamuzi baada ya pande zote husika kusikilizwa.

Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga, alisema jana kuwa watakutana na kutafakari hatua zaidi za kuchukua.

“Kufungiwa kwa Mwanahalisi kunathibitisha kwamba serikali bado ina ‘shauku’ ya kufungia vyombo vya habari licha ya kupitishwa kwa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016,” alisema Makunga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles