Mwandishi Wetu- Serengeti
SERIKALI imeanza ukaguzi wa hoteli za kitalii ilizozibinafsisha kwa wawekezaji na wale watakaobainika kuziendesha chini ya kiwango, watanyang’anywa na kupewa wawekezaji wengine.
Hatua hiyo, inafanyika kutokana na kuwapo malalamiko kutoka kwa watalii na wadau mbalimbali wa utalii juu ya huduma zisizoridhisha zinazotolewa na hoteli hizo.
Akizungumza baada ya kukagua baadhi ya hoteli hizo,zikiwamo Soronera na Lobo, zilizo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu alisema lengo la kubinafsishwa hoteli hizo ilikuwa ni kuboresha huduma.
Alisema hata Hoteli ya Musoma na Ngorongoro Wildllife iliyopo ndani ya Mamlaka ya Eneo la Ngorongoro, ni miongoni mwa hoteli zilizofanyiwa ukaguzi.
Alisema mwekezaji asiyefanya hivyo, atanyang’anywa umiliki ili apewe mwekezaji.
Alisema kumekuwa na tuhuma kwa baadhi ya hoteli zilizobinafsishwa kukwepa kodi ya tozo ya huduma pamoja na kuwalipa wafanyakazi wazawa mishahara midogo, huku wale wa kigeni wakilipwa mishahara mikubwa kwa kazi ya aina moja.
Akizungumza baada ya kukagua hoteli hizo,Waziri Kanyasu alisema baadhi vitu alivyoviona ni pamoja na uchakavu wa miundombinu na udanganyifu wa idadi ya watalii wanaofikia kwenye hoteli hizo .
Alisema wizara itapeleka idadi ya hoteli zitakazobainika kwenda kinyume ili Msajiri wa Hazina aweze kuzifutia umiliki.
Kuhusu tozo ya huduma ya mapato, amezielekeza halmashauri mbalimbali, ikiwemo ya Serengeti kupata taarifa sahihi kutoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa ( TANAPA)
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti,Victor Tonesha alisema changamoto inayoikabili halmashauri hiyo, ni ya kushindwa kubaini kiwango halisi cha fedha zinazotolewa na Wawekezaji hao.