Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, ameagiza kuundwa kamati kila mkoa, ambao itashirikiana na taasisi nyingine za Serikali kusimamia miradi mbalimbali ili kuepuka kuwaingizia hasara wananchi na Serikali.
Hatua hiyo inatokana na hoja iliyotolewa juzi na Mchungaji wa Kanisa la Baptist, Daniel Mgogo wakati wa mkutano wa mwaka wa mashauriano uliowahusisha wakandarasi, wahandisi na wabunifu majengo.
Mchungaji huyo alimweleza Rais Dk. John Magufuli masikitiko yake kwa wananchi kuvunjiwa nyumba zao kwa madai ya kujenga eneo la barabara ilihali waliojenga ni wakandarasi waliosoma na kujua sheria, na Serikali inawapelekea huduma za maji, umeme, barabara na nyinginezo.
Alisema Serikali kupitia taasisi zake, ingekataa kupeleka huduma hizo maeneo inayojua ni hifadhi ya barabara ama yenye matumizi mengine, wananchi wasingejenga.
Akizungumza jana wakati wa kufunga mkutano huo, uliozihusisha Bodi za Usajili wa Makandarasi (CRB), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Kamwelwe alisema kamati hizo zitakuwa zinakutana mara moja kwa mwezi.
“Kama una mradi wa Rea, maji au barabara unamweleza mwenzako utapita maeneo gani ili makosa yasijirudie. Mradi wa TTCL tulijenga kwa mabilioni, lakini baada ya miaka mitatu tulilazimika kufukua nyaya na tukatoa fedha kufidia, sasa huu si uharibifu wa fedha?
“Ubungo hati zaidi ya 28 zilitolewa na Serikali kwenye ‘road reserve’, tumejifunza je, tuendelee kukosea jamani?” alihoji Kamwelwe.
Pia alizielekeza taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo kuhakikisha katika miradi mikubwa, kuanzia tangazo la zabuni wakandarasi wazawa wanashirikishwa.
“Katibu Mkuu ataunda jopo la wataalamu ili waweze kupitia upya sheria na kuainisha kama kuna vipengele vya kufanyiwa marekebisho na hili lifanyike ndani ya mwezi mmoja,” alisema.
Mwenyekiti wa ERB, Profesa Ninatubu Lema, aliiomba Serikali iendelee kuwatumia wataalamu hao katika nyanja mbalimbali za ujenzi wa miundombinu.
Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani (CCM), aliwataka wataalamu hao kuanza kujikagua wapi ambako hawafanyi vizuri na kutoa mchango wao kufikia uchumi wa viwanda.
“Nani hajui kwamba kuna barabara tunajenga lakini zinaharibika katika hatua za awali, kama utajenga chini ya kiwango unawezaje kumshawishi asichukue mtu mwingine ambaye hana utaalamu kama wako, lakini anajenga vizuri?” alihoji Makani.