Na Derick Milton, Simiyu
Siku chache baada ya kuripotiwa taarifa ya Mama Zawadi Sayi Abdallah mkazi wa Kidinda Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu kudai kuwa alijifungua mapacha lakini akapewa mtoto mmoja. Serikali imeingilia kati tukio hilo na kueleza kuwa utafanyika uchunguzi wa kina ambao utavihusisha vyombo vya kiuchunguzi ili kuweza kupata ukweli wa jambo hilo ambalo bado limegubikwa na mashaka mengi.
Kupitia vyombo vya habari, mwanamke huyo aliwalalamikia wahudumu wa afya katika hospitali ya halmashauri hiyo (Somanda) kumpatia mtoto mmoja badala ya watoto wawili (mapacha) baada ya kufika hapo na kujifungua.
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkuu wa Wilaya hiyo Lupakisyo Kapange alisema kuwa bado kuna mashaka juu ya jambo hilo licha ya uchuguzi wa awali kuonyesha kuwa mama huyo alijifungua mtoto mmoja.
“Kama Mkuu wa Wilaya nitafika kwenye familia ambayo inalalamika kuonana nao, ili waniambie ukweli na kama kweli wanaridhika na huu uchunguzi wa awali, au bado wana mashaka, ili tukubaliane na kila mtu aridhike kwa haki,” alisema Kapange nakuongeza kuwa:
“Ukirudi kwenye nyaraka zinasema mtoto ni mmoja, wao wanalalamika wanasema kuna mhudumu aliwaambia alijifungua watoto wawili, kama bado wataendelea kuwa na mashaka kama mkuu wa Wilaya nitaagiza uchunguzi wa kina ufanyike,” aliongeza Kapange.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa ikiwa familia hiyo itaendelea kuwa na mashaka, vyombo vyote vya kiuchunguzi vitalazimika kutafuta ukweli wa jambo hilo kwa pande zote mbili.
Alisema kuwa taarifa zote tangu mama huyo ameanza kwenda kliniki, hakuna sehemu ambayo inaonyesha kuwa alikuwa na mapacha, na wakati wa kujifungua nayaraka zote zinaonyesha ni mtoto mmoja.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya ameagiza kufanyika uchunguzi kwa mmoja wa watoa huduma ambao walimhudumia mama huyo ambaye anadaiwa kupokea kiasi cha sh. 20,000 kutoka kwa mlalamikaji.
“Mtoa huduma huyo aandike maelezo ya kwanini aliomba na kupokea kiasi hicho, ni kwa ajili ya nini, je? Alitoa stakabadhi? Lakini ufanyike uchunguzi mweingine kujua nani alikwenda kwenye familia hiyo kuwatisha,” alisema Kapange.
Alisema kuwa vitu hivyo ndivyo vinaendelea kutiliwa mashaka ya kuwa jambo hilo linawezekana kuwa na ukweli licha ya nyaraka kuonyesha hakuna ukweli na vinaweza kupelekea jambo hilo kushindwa kufikia mwisho.
Naye Mkurugenzi wa halmashuari hiyo Merkzedeck Humbe alisema kuwa kuna haja ya kufanyika kwa uchunguzi wa kina kujua ukweli sahihi wa jambo hilo kwa pande zote mbili ili kila upande uweze kupata haki yake.
“Nyaraka zinasema mambo mengine, lakini wahusika nao wanasema mambo mengine, hapo kuna haja ya uchunguzi wa kina kufanyika kama ambavyo Mkuu wa Wilaya amesema ili jambo hilo liweze kufikia mwisho,” alisema Humbe.
Kuhusu mlalamikaji kutakiwa kununua dawa na vifaa tiba ili afanyiwe upasuaji, Mganga mkuu wa Halmashuari, Judith Ringia alisema kuwa mama huyo baada ya kupewa orodha ya vifaa vinavyohitajika hakupita dirisa la dawa.
“Suala hili tumegundua mama huyu hakupita dirisha la dawa, alipitiliza moja kwa moja, na alipofika kwenye duka letu la ndani ya hospitali alikuta bei ni kubwa ndiyo akaamua kwenda moja kwa moja nje ya hospitali kwenye maduka ya watu binafsi,” alisema Ringia.
Malalamiko
Kwa mujibu wa Zawadi, licha ya kupewa mtoto mmoja baada ya kujifungua na kuondoka kurudi nyumbani akiwa ameridhika alishangaa kupata taarifa mpya kutoka kwa mhudumu mmoja ambaye alimweleza kuwa alijifungua watoto wawili.
“Wiki mbili baada ya kupita tangu nitoke hospitali, nilirudi hapo hospitalini kwa ajili ya kusafisha kidonda, ndipo huyo mhudumu akanipa hizo taarifa, nikaunganisha na zile ambazo mhudumu wa kwanza alinipatie wakati wa vipimo, nikaona kuna ukweli,” alisema Zawadi.
Kuhusu kununu dawa na vifaa tiba, Zawadi anasema kuwa siyo kweli kuwa alipitilisha dirisha la dawa, bali alikwenda kwenye hilo dirisha wakwambia kuwa vifaa vyote havipo, akaelekea duka la ndani akakuta bei ni kubwa ndipo akatoka nje ya hospitali.