Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Serikali imefuta zaidi ya tozo 374 na kurekebisha zaidi ya sheria na kanuni 55 katika kipindi cha mwaka 2017/18 na 2022/23 kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (Mkumbi).
Kufutwa kwa tozo hizo ni matokeo ya utekelezaji wa mradi wa Begin ambao unalenga kukuza uchumi, ajira na ubunifu kwa vijana na wanawake kupitia kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza usalama wa mlaji na kuwawezesha wajasiriamali wakubwa, wa kati na wadogo kuzingatia ubora wa bidhaa.
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 22,2024 baada ya mkutano wa kamati tendaji ya mradi wa Begin, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dk. Tausi Kida, amesema kipaumbele katika tozo hizo ni katika sekta za uwekezaji, kilimo, mifugo na uvuvi, maliasili, utalii, nishati, madini, viwanda na biashara.
“Matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika kutoa huduma mbalimbali ikiwemo leseni, vibali na ada. Uwepo wa ukaguzi wa pamoja kwa taasisi za udhibiti na kupungua kwa idadi ya siku za kupata hii ni kutokana na matumizi ya kielektroniki katika taasisi za umma katika kutoa huduma,” amesema Dk. Kida.
Aidha amesema uanzishwaji wa mdumo wa dirisha moja la huduma yaani Tanzania Electronic Investment Window (TeIW) unawezesha wawekezaji kupata huduma mahali pamoja.
Kuhusu mradi wa Qualitan ambao unatekelezwa na Unido amesema umefanikiwa kutoa mafunzo ya ndani na nje ya kuwajengea uwezo wataalam wa Shirika la Viwango (TBS) na sasa wanaweza kuwasilisha maombi ya kutambuliwa kwa huduma zake kwa bodi za kimataifa zinazosimamia viwango.
Akizungumzia programu ya ubunifu ya Funguo inayotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (Undp) kwa kushirikiana na Serikali ya Uingereza amesema imefikia kampuni changa za kibunifu 1,800 ambapo Sh bilioni 4 zimetolewa kwa kampuni 43 za vijana ambao wamewezeshwa kutoka hatua moja kwenda nyingine.
“Mwaka 2023 kampuni zilizopata ufadhili zimechangia kutengeneza ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja 4,000 kwa vijana wa kike na kiume,” amesema.
Mwakilishi kutoka UNDP, Shigeki Komatsubaki, amesema programu hiyo italeta matokeo chanya kwa vijana na kuwawezesha kukuza bunifu zao kwa maendeleo endelevu.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka UNIDO, Dk. Victor Djemba, amesema mpango huo umefanya vizuri katika maeneo mbalimbali hasa katika bunifu za vijana.
Mradi wa Begin unajumuisha makatibu wakuu kutoka wizara za kisekta, mwakilishi wa Umoja wa Ulaya nchini, watendaji wakuu kutoka mashirika ya kimataifa ya UNIDO na UNDP.
EU imetoa Sh bilioni 63.5 ambazo zimeelekezwa kufadhili Mkumbi na fedha hizo zimeelekezwa katika mradi wa Qualitan ambao umejikita kuimarisha maabara za TBS na nyingine katika mradi wa UNDP Funguo ambao unawezesha kampuni changa zinazochipukia.