30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAFUTA POSHO KWA WATUMISHI WA UMMA

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM


 

kassim-majaliwaWAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa posho mbalimbali zisizokuwa za kisheria zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Agizo hilo alilitoa jana Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi.

“Kuanzia sasa marufuku wakurugenzi kutoa posho zisizotambulika kisheria zikiwamo za mazingira magumu, kujenga uwezo na vitafunwa katika halmashauri zenu na badala yake fedha hizo zitumike kwenye miradi ya maendeleo,” alisema.

Agizo hilo litawezesha Jiji la Dar es Salaam kuokoa Sh bilioni 130 zilizokuwa zitumike na halmashauri na manispaa za jiji hilo, ambazo kwa sasa zitaingizwa katika miradi na shughuli za maendeleo.

“Sasa hivi madiwani hakuna kupewa fedha za miradi ya maendeleo mkononi, bali wawasilishe vipaumbele vya miradi yao ili halmashauri husika isimamie malipo yake kwa ajili ya kuepuka migogoro.

“Madiwani kama mna kampuni haziruhusiwi kufanya kazi katika halmashauri mlizopo ili kuondoa upatikanaji wa zabuni za upendeleo, kitendo kinachoshusha ufanisi wa kazi,” alisema.

Katika hatua nyingine, waziri mkuu alizitaka halmashauri zote nchini kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya kodi na yasiyo ya kodi.

“Serikali itaendelea kuongeza kiwango cha ruzuku kwa halmashauri zote nchini kulingana na bajeti itakavyoruhusu, tunataka halmashauri zitekeleze miradi yake ipasavyo,” alisema.

Pamoja na hali hiyo. amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuacha kutumia fedha kinyume cha utaratibu na watakaobainika Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali za kisheria.

“Katika halmashauri zetu kila mtumishi anashiriki katika ukusanyaji wa mapato, hadi walinzi. Lakini mwisho wa siku vitafunwa huliwa na wachache wanaojiita wakubwa, huku wengine wakisikilizia kwa nje. Jambo hili haliwezekani,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alisisitiza kwamba mkurugenzi yeyote atakayebainika kulipa posho hizo baada ya siku ya jana   atakuwa amejifukuzisha kazi.

Aliagiza fedha zilizokuwa zikitolewa kwa madiwani kuhamasisha maendeleo zisitolewe moja kwa moja kwa madiwani na badala yake zipelekwe katika kata husika na zifuatiliwe matumizi yake.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amezionya halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa kila fedha zinayopelekwa kwenye halmashauri hizo inatumika kama ilivyokusudiwa na atakayebainika kutumia kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Pia aliwataka watumishi wote wa umma nchini kuwajibika ipasavyo na kuhakikisha wanawatumikia vyema wananchi, ikiwa ni pamoja na kuepuka vishawishi na kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na ufisadi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa siku tatu kwa watumishi 10 wa Halmashauri ya Kigamboni ambao wamehamishiwa kutoka Wilaya ya Temeke wawe wameripoti, vinginevyo watakuwa wamejifukuzisha kazi.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa, wakati akiwasilisha taarifa ya wilaya hiyo kwa Waziri Mkuu, alisema hadi sasa asilimia 98 ya watumishi waliotakiwa kuhamia kwenye halmashauri hiyo wameripoti isipokuwa 10 na hakuna taarifa zozote juu yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles