Na Michael Sarungi
CHAMA cha Masoko ya Fedha ya Ndani na Nje tawi la Tanzania (ACI), kimetoa wito kwa Serikali kupunguza manunuzi ya bidhaa zisizokuwa na umuhimu kwa kutumia dola kutoka nje ili kukabiliana na anguko la shilingi ya Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Rais wa chama hicho tawi la Tanzania, Ivan Tarimo toka katika Benki ya Stanbic, alisema kwa kiwango fulani Serikali imechangia kushuka kwa thamani ya shilingi.
Alisema kitendo cha Serikali kuziruhusu baadhi ya taasisi zake kuagiza bidhaa kama samani za ndani zinazopatikana hapa nyumbani kutoka nje kwa kutumia dola ni sawa na kuihujumu shilingi ya Tanzania.
Alisema anguko la shilingi halikuja kwa bahati mbaya, bali limetengenezwa na Serikali na kusisitiza kuwa tusitafute mchawi.
“Huwezi ukatarajia kuimarika kwa shilingi yako wakati huo wewe unategemea kununua toka nje tu na hakuna unachokiuza wala kuzalisha,” alisema Tarimo.
Alisema ni kweli katika miezi ya hivi karibuni uchumi wa Marekani umeimarika, lakini hicho kisiwe kisingizio cha kuanguka kwa shilingi yetu.
Tarimo alisema tabia ya kuruhusu matumizi ya dola hata pasipostahili haijaanza leo wala jana, bali ipo kwa muda mrefu.
“Kama nchi tumefika mahala tuanze kujiuliza maswali magumu juu ya nini cha kufanya kuikomboa thamani ya shilingi yetu, vinginevyo huko tuendako hali si nzuri,” alisema Tarimo.
Kwa upande wake, Mweka Hazina mkuu wa benki ya NBC, Azizi Chacha, alisema kama nchi, inatakiwa tuanze kuzalisha bidhaa tunavyoweza kwa ajili ya kuuza nje ili kuimarisha uchumi.
Alisema hakuna nchi yoyote duniani iliyopata maendeleo kwa kukubali kuwa dampo la bidhaa kutoka nje, tena nyingi zikilalamikiwa na walaji kuwa havifai.
“Hebu pita kwenye maduka mengi hapa nchini, vitu vingi tunavyouza ni kutoka nchi za nje, halafu utegemee shilingi kuwa imara?” alisema Chacha.