28.4 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaanika matumizi ya mitandao

IMG_0131NA ESTHER MNYIKA, DAR ES SALAAM

SERIKALI imetoa takwimu zinazoonyesha jinsi watumishi wa serikali wanavyotumia muda mwingi wa kufanya kazi kuperuzi mitandao ya kijamii.

Imesema imefanya uchunguzi na kubaini kuwa watumishi wengi wa serikali hutumia muda wa kazi kuperuzi mitandao ya kijamii kwa shughuli zao binafsi, huku wakiacha kutoa huduma kwa wananchi pamoja na kutekeleza majukumu yao.

Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alipokuwa akizungumzia na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Makumbusho, Dar es Salaam.

Waziri Mbarawa alisema wizara yake imefanya uchunguzi wa matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watumishi wa serikali na kubaini kuwa megabaiti zinazotumika katika taasisi mbalimbali za serikali hazitumiwi katika matumizi halali.

Alisema asilimia saba pekee ndiyo iliyobainika kuwa matumizi halali, huku asilimia 27 zikitumiwa na wafanyakazi wa serikali kupakua (kudownload) vitabu vya shule kwa ajili ya watoto wao.

Waziri huyo alisema asilimia 20 zimabainika kutumika kupakua (kudownload) video alizosema kimsingi hazina uhusiano na utendaji kazi wa watumishi wa serikali na asilimia 37 zinatumika kutumiana mafaili mengine yasiyo na umuhimu katika utendaji kazi.

“Suala la kuchati maofisini limekuwa ni ugonjwa ambao unahitaji kuondolewa haraka na nieleweke kuwa sisemi kuwa tuondoe matumizi ya mitandao, lakini kiuhalisia tupunguze kuchati kazini.

“Tumebaini kuwa megabaiti zinazotumika katika taasisi mbalimbali za serikali hazitumiwi katika matumizi halali, asilimia saba pekee ndiyo matumizi halali, asilimia 27 zikitumika kudownload vitabu vya shule kwa ajili ya watoto wao, asilimia 20 kudownload video ambazo kimsingi si katika masuala ya kazi, 37 nyingine wanatumia katika kutumiana mafaili mengine yasiyo na umuhimu,” alisema Waziri Mbarawa.

Alisema amekutana na wafanyakazi wa wizara yake jana kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo na kuwataka kubadili mwenendo wao na kujiepusha na matumizi ya mitandao yasiyotakiwa katika ofisi za umma.

“Tumekutana hapa leo na wafanyakazi wote ili kufahamiana, maana tangu wizara hii iunganishwe ni mara yetu ya kwanza kukutana, sasa tunahitaji wafanyakazi kuwa na kasi kubwa ya kufanya kazi katika awamu hii, tufanye kazi kweli ili wizara hii iwe mfano wa kuigwa na wizara nyingine.

“Wizara hii ina taasisi 29 zinazohitaji kufanya kazi kwa ushirikiano na wizara ili kuhakikisha inafikia malengo mahususi. Tufahamu wizara yetu ndiyo itakayofikisha Watanzania katika uchumi wa kati kwa kuboresha miundombinu, hivyo ni jukumu letu kuwajibika inavyotakiwa,” alisema Waziri Mbarawa.

Wakati huo huo, Waziri Mbarawa alisema kuwa serikali inakusudia kuanza kukusanya Sh trilioni moja zinazotokana na malipo ya kodi kila mwezi kutoka Mamlaka ya Bandari (TPA).

“Tunaanza na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha wanakusanya kodi itakayofika Sh trilioni moja kwa mwezi, awali walikuwa wakikusanya zaidi ya bilioni 600, sasa tufahamu TPA ni taasisi kubwa, endapo watashindwa kukusanya kiasi hicho kwa mwezi basi mkurugenzi ataondolewa na kutafutwa mwingine haraka na suala hili si kwa bandari tu, bali ni kwa taasisi zote zilizopo kwenye wizara yetu,” alisema Waziri Mbarawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles