26.1 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaajiri vijana 1,000

Nora Damian-Dar es Salaam

ZAIDI ya vijana 1,000, wamepata ajira kupitia programu ya taifa ya mafunzo kwa vitendo inayoendeshwa mahala pa kazi kwa vijana waliohitimu katika vyuo mbalimbali.

Utafiti wa Nguvu Kazi Tanzania uliofanyika mwaka 2018, unaonyesha vijana wenye uwezo wa kufanya kazi ni milioni 15.7, lakini asilimia 9.7 hawana ajira.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, alisema vijana wengi wana uwezo wa kuajiriwa lakini hawana uzoefu.

Jenista alikuwa akizungumzia mkutano wa mawaziri wa masuala ya kazi na ajira katika Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaoanza leo nchini.

“Kila baada ya miaka mitano tunafanya utafiti kujua hali ya nguvu kazi tuliyonayo kwa sababu programu yoyote lazima itokane na utafiti.

“Mwaka 2014, ukosefu wa ajira ulikuwa asilimia 10.3, lakini mwaka 2018 umeshuka hadi asilimia 9.7, tunapigana twende kwenye ‘digit’ moja, tunataka ishuke zaidi,” alisema Jenista.

Kwa mujibu wa Jenista, kupitia programu hiyo mafunzo hutolewa kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja na imewafikia vijana 5,000 na wengine 14,000 wameomba.

“Programu hii, itaondoa kigezo cha kutokuwa na sifa ya uzoefu kwa vijana wanaotaka kazi, vijana watapata ujasiri wa kimtazamo, kujiajiri na kuajiri wenzao.

“Kuna tovuti ambayo vijana wenye utaalamu mbalimbali na wenye vyeti vilivyotambulika na kufanyiwa ithibati wanajisajili na kuweka CV zao, halafu tunawapanga kulingana na mahitaji ya makundi ya waajiri,” alisema.

Alisema pia kuna mfumo wa mawasiliano na waajiri wote wamepatiwa mafunzo maalumu kuhakikisha vijana walio kwenye programu hiyo wanafikia malengo yao.

Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Ukuzaji Ajira, Robert Masingiri alisema kiwango cha nguvu kazi chenye ujuzi wa chini nchini ni asilimia 79.9 na malengo ya Serikali ni kuhakikisha hakizidi asilimia 54 ambayo ni viwango vya kimataifa.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kiwango cha ujuzi wa kati ni asilimia 16 na malengo ni kukipandisha hadi kufikia asilimia 34 huku kiwango cha juu ambacho ni asilimia 3.6 kipande hadi kufikia asilimia 12.

Alifafanua kuwa programu hiyo inawalenga vijana waliohitimu kuanzia ngazi ya stashahada na Serikali hushirikiana na waajiri husika kuwawezesha vijana wakati wanapokuwa kwenye mafunzo hayo.

Kuhusu mkutano huo, Waziri Jenista alisema utazinduliwa Alhamisi na Makamu wa Rais, Samia Suluhu, sambamba na programu hiyo.

Alisema mpaka sasa mawaziri 10 kutoka nchi wanachama, wamethibitisha kushiriki ambao wataambatana na vyama vya wafanyakazi na waajiri.

Alisema miongoni mwa masuala yatakatojadiliwa, ni uimarishaji wa nguvu kazi ili kuona kama kila nchi inaweza kuchukua uzoefu na kuupeleka nchi nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles