29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YA JPM YAPEWA DARASA ZITO LA VIWANDA


Na MWANDISHI WETU      |  

MJADALA ulioshuhudiwa bungeni wiki hii, wakati wabunge wakipitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa fedha wa 2018/19, huenda ukawa umetoa darasa jingine jipya kuhusu agenda ya ‘Tanzania ya Viwanda’ inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Mjadala wa sasa, ambao umebeba hoja ambazo si mpya sana, umechagizwa zaidi na migogoro ya mafuta na sukari, iliyoibuka hapo kabla, lakini pia kuporomoka kwa masoko nje ya nchi.

Hoja zilizoibuliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ndani na nje ya Bunge na baadaye Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe kuhusu viwanda, uwekezaji, gharama za kodi na kuporomoka kwa masoko nje ya nchi, ndizo ambazo zinaweza kuthibitisha kile ambacho baadhi wanaona si tu kama darasa, bali ushauri kwa Serikali iliyojipambanua kuibeba agenda ya viwanda.

Kauli ya ukali ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa mawaziri akiwataka kutoa majibu yanayoridhisha kuhusu mgogoro wa mafuta ya kula ulioibuka wiki hiii, lakini pia akitaka utaratibu mpya wa safari za nje kwa mawaziri, yote hayo yametoa taswira hiyo hiyo.

Baadhi ya hoja ambazo wafuatiliaji hao wanaona hazipaswi kuendelea kuachwa au kupuuzwa katika kufanikisha agenda hiyo ya viwanda ni ile ya kufungamanisha sekta ya kilimo na viwanda, ambayo Zitto anaona ndiyo njia sahihi ya kutatua migogoro mingi ya kale, ambayo imekuwa ikiibuka mara kwa mara, ikiwamo sukari na mafuta ya kula.

Akichangia bungeni wiki hii na katika andiko lake, Zitto, ambaye amekuwa akieleza hoja hiyo tangu mwaka 2016, alisema huo ndio mkakati pekee wa kupambana na tatizo hilo, kwani itaongeza thamani ya mazao ya wakulima na kuhakikisha viwanda vinavyoanzishwa vitategemea kwa kiasi kikubwa malighafi kutoka ndani ya nchi, hasa bidhaa za kilimo.

Katika hesabu zake, anasema iwapo jambo hilo lingetekelezwa, ziada ya sukari ambayo ingeuzwa nje ingeweza kuliingizia Taifa fedha za kigeni, dola za Marekani milioni 500, sawa na asilimia 30 ya malengo ya Mpango wa Maendeleo kwa sekta ya viwanda, wa kupata mapato ya fedha za kigeni, kiasi cha dola za Marekani bilioni tatu.

Zitto alishangaa hoja hiyo kupuuzwa na kusema huo ndio msingi wa migogoro inayoshuhudiwa sasa, kwani bado hakuna mpango wa Taifa wa namna ya kufidia nakisi ya sukari itokanayo na uzalishaji mdogo wa bidhaa hiyo nchini.

“Matamko ya zuio ya Rais yaliishia kuleta uhaba wa sukari na kupandisha bei kutoka Sh 1,800 mpaka Sh 6,000 katika maeneo mbalimbali nchini, na tangu hapo bei ya sukari haijashuka tena, imebaki kuwa 3,000 kwa kilo,” alisema Zitto.

Alisema uhitaji wa sukari nchini ni mkubwa, kwani mwaka 2016/17 utafiti uliofanywa na Bodi ya Sukari kwa kutumia kampuni ya LMC International, ulibaini mahitaji ya sukari ni wastani wa tani 590,000 na kati ya hizo, tani 455,000 ni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na tani 135,000 kwa matumizi ya viwandani, lakini tayari mwaka 2018 nakisi hiyo ya mahitaji ya sukari imekua zaidi.

Kuhusu mafuta ya kula, Zitto alisema Serikali ingekubali ushauri wa mwaka 2016, isingetumia fedha nyingi ambazo alidai ni kiasi cha Bajeti ya Wizara ya Maji 2018/19 ili kuagiza nje ya nchi.

Alisema msingi wa tatizo la mafuta ya kula halina tofauti na lile la sukari, kwani utatuzi wake si unafuu wa kodi kwa mafuta yanayoagizwa kutoka nje ambao Serikali iliutoa kwa waagizaji nchini.

Alisema unafuu huo ulivunja hamasa ya uwekezaji wa viwanda vya kuzalisha mafuta ya kula ndani ya nchi.

Alisema wakati ule wa Bajeti ya mwaka 2016/17, waliishauri Serikali iondoe unafuu huo wa kodi inaoutoa kwa waagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje, ili kulinda na kunusuru viwanda vya ndani, jambo ambalo lilitekelezwa mwaka huu na hivyo kupoteza zaidi ya mwaka na kuathiri viwanda vya ndani.

Alisema kwenye uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula, mwaka jana ulikuwa ni tani 180,000 tu, wakati mahitaji yalikadiriwa kuwa ni tani 400,000 mpaka tani 520,000 kwa mwaka.

Alisema ili kujazia nakisi ya uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula, nchi inatumia sehemu kubwa ya akiba yake ya fedha za kigeni kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

Alisema kwa wastani, kwa mwaka taifa linatumia dola za Marekani 340 milioni, sawa na Sh bilioni 782, ambazo ni zaidi ya Bajeti yote ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka 2018/19, ambayo ni Sh bilioni 727.

Mbali na hayo, kuhusu hali ya uchumi, Zitto alizungumzia biashara ya nje, akisema kwa miezi 24 iliyopita, Serikali imesababisha hasara ya mauzo ya nje ya thamani ya dola bilioni moja.

Akitolea mfano, alisema mauzo ya Tanzania nchini China yameporomoka kutoka dola milioni 356 mwaka 2016 hadi dola milioni 217 mwaka 2017 na Japan yameporomoka kutoka milioni 140 hadi dola milioni 75.

Zaidi Zitto alizungumzia kitendo cha Tanzania kushindwa kuuza mbaazi, dengu, choroko na giligilani nchini India na hivyo kupoteza mamilioni ya fedha.

Katika hilo, Zitto alimshauri Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, kutoka nje ya nchi kutatua matatizo kama hayo.

Kauli hiyo ya Zitto iliungwa mkono na Spika wa Bunge, Job Ndugai, ambaye alisema ni lazima mawaziri wasafiri.

Akizungumzia mipango ya Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kama vile reli, barabara, ndege, madaraja, mabomba ya gesi na mafuta, Zitto alionyesha wasiwasi fedha nyingi kuishia nje ya nchi.

Alisema mradi wa reli ya kati kwa kiwango cha SGR unahitaji wastani wa Sh trilioni 17 ili kukamilisha ujenzi wake kati ya Dar es Salaam na Mwanza (1,200km) na kwamba vitahitajika vyuma vya pua si chini ya tani 500,000 kwa kipindi cha miaka michache ijayo.

Alisema mataruma ya reli yataagizwa kutoka nje na kuletwa nchini na hivyo kuzalisha ajira nje ya nchi, huku pia fedha za miradi hiyo zikienda nje ya nchi, kama ilivyo kwenye fedha za mafuta ya kula na sukari.

Katika hilo, Zitto alihoji iwapo Serikali imeweka mikakati ya kufungamanisha maendeleo ya viwanda na miradi hiyo.

Kwa maoni yake, alisema jambo hilo lingeweza kufanyika nchini, kwa kuwa kuna chuma kingi Mchuchuma na Liganga, na makaa ya mawe ya kuchenjua chuma ili kupata chuma cha pua (steel), hivyo mradi wa reli ungeweza kuchochea maendeleo makubwa kwenye sekta ndogo ya migodi na viwanda vya chuma.

Alisema Tanzania ingeweza kuwa mzalishaji mkubwa wa chuma eneo la Mashariki mwa Afrika na Maziwa Makuu, huku bidhaa za ngozi na mkonge zikitumika kutengeneza vitanda na viti vya mabehewa ya treni.

Kwa upande wake, Mbunge wa Nzega Mjini, Bashe, alisema mfumo wa kodi nchini umesababisha gharama za uzalishaji bidhaa kuongezeka na kudumaza mazingira rafiki ya uwekezaji.

Aliitaka Wizara hiyo kukutana na Wizara ya Fedha na Mipango ili kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji yatakayomsaidia Rais John Magufuli kutimiza ndoto ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

“Muujiza wa kwanza ulikuwa ni kuona namna gani Wizara ya Viwanda inaweza kuunganisha mambo matatu ambayo amekabidhiwa. Rais aliamua kwa makusudi kuunganisha biashara, viwanda na uwekezaji ili kufikia lengo la mapinduzi ya viwanda.

“Lakini hadi leo tunazungumzia General Tyre, Liganga na Mchuchuma. Kuna matatizo ya msingi ya biashara, lakini huoni kwenye mpango wetu namna ya kuyashughlikia,” alisema Bashe.

Alisema hakuna mpango unaoonesha kuondoa matatizo yaliyopo kwenye mifumo ya kodi, miongozo na sheria katika kufanya biashara nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles